Na: Farida Mkongwe
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amezindua Jengo Mtambuka la Mafunzo
lililopo katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na kukipongeza Chuo
hicho kwa kufanya tafiti zenye tija nchini na kutoa majibu kwa mahitaji ya
jamii za Tanzania na Afrika.
Akizindua Jengo hilo Agosti 6,
2024 lililojengwa kwa thamani ya Sh. Bilioni 11.7 lenye Maabara 8 na Madarasa 8
yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 3205 kwa wakati mmoja, Rais Samia
amekipongeza Chuo Kikuu cha SUA kwa kukamilisha jengo hilo kwa ufanisi mkubwa
na kukubali kutoa zaidi ya Sh. Bilioni 2.6 ili kufanikisha ujenzi huo ambapo
Serikali imetoa Sh. Bilioni 9 kati ya Sh. Bilioni 11.7 .
“Niseme kwa ukweli nimelemewa na performance ya hapa nilipokuja kuweka
jiwe la msingi ilikuwa ni matofali na machuma chuma, pamoja na kwamba
nilioneshwa majengo kwenye ramani wakati wananipitisha kunionesha jengo
litakuwaje lakini sidhani kama niliamini leo nitakuja kukuta kitu cha aina hii
niwapongeze sana sana sana SUA kwa kazi hii nzuri mliyofanya, lakini pia
niipongeze Menejimenti ya SUA ama kwa hakika mmefanya kazi nzuri, asanteni
sana”, amesema Mhe. Rais Samia.
Rais Samia pia amekipongeza Chuo
Kikuu cha SUA kwa kuwa na Maabara hizo mpya zenye ithibati ya kimataifa hali
inayopelekea tafiti zinazofanyika kukubalika ulimwenguni kote huku akikipongeza
pia kwa kuendelea kufanya tafiti zenye tija, kuzalisha wataalam wanaoendelea
kuhudumia jamii pamoja na kufundisha wanafunzi wa kigeni kutoka nchi mbalimbali
na kusema kuwa hiyo ni fahari kwa Tanzania .
“Pia nisema kuwa haya
yanayoendelea SUA mnaelekea kwenye kutoa majibu kwa mahitaji ya jamii, mahitaji
ya kwanza ajira lakini la pili tafiti mbalimbali zitakazotoa majibu kwa
wakulima zinafanyika hapa SUA lakini lingine ni mafunzo kwa vikundi mbalimbali
vya nje kuja kujifunza hapa SUA sasa kwa hapa kwa sababu tuna wageni kutoka
nchi mbalimbali basi niseme mnatoa majibu pia kwa nchi nyingine ndani ya Afrika
, hili nalo nataka niwapongeze sana SUA”, amepongeza Mhe. Samia.
Rais Samia amezindua Jengo hilo
ikiwa ni miaka mitano imepita tangu alipoweka jiwe la msingi akiwa ni Makamu wa
Rais Agosti 7, 2019.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha
Mhe. Rais Samia, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda
amesema Serikali inajivunia sana kazi nzuri za tafiti zinazofanywa na SUA ikiwa
ni pamoja na tafiti zilizowezesha kupatikana kwa chanjo ya kuku dhidi ya
ugonjwa wa mdondo au kideri na utafiti wa mbegu bora ya maharage inayoitwa
Mshindi ambayo inahimili ukame na kustahimili magonjwa .
“Mhe. Rais kuhusu changamoto ya
ufadhili ipo, nakumbuka ulitwambia wakati tunapotoa vivutio tuwaangalie na
Wahadhiri wa vyuo vikuu ambao wanatumia muda mrefu sana kwa ajili ya kufanya
utafiti, tayari tumeanza kutoa tuzo ya Sh, milioni 50 kwa Mtafiti yeyote ambaye
utafiti wake utakubalika kimataifa na kigezo cha kimataifa ni kuchapisha
majarida ya hali ya juu zaidi duniani, lakini niseme tu ili kuweza kushikilia
agenda ya tafiti hatuna budi kutafuta fedha kwa ajili ya kuwawezesha watafiti
nchini”, amesema Prof. Mkenda.
0 Comments