SUAMEDIA

Wakulima watakiwa kutumia taarifa sahihi na kusoma machapisho ili kuzalisha kwa tija

  

Na: Farida Mkongwe

Wakulina nchini wametakiwa kutumia taarifa na machapisho mbalimbali yaliyopo kwenye Maktaba ya Taifa ya Sokoine ya Kilimo (SNAL) ambayo yapo kwenye lugha nyepesi ya Kiswahili ili waweze kulima kwa tija na kuongeza uzalishaji.

                                    


Wito huo umetolewa na Mkutubi wa Maktaba ya Sokoine ya Kilimo Moses Kahale wakati akizungumza na SUA Media katika banda la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwenye Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yanayofanyika katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere mjini Morogoro.

                                  

Bw. Kahale amesema mwaka huu 2024 wameongeza idadi ya vitabu na machapisho ambayo yametayarishwa na wataaalamu kutoka SUA na vitabu vingine ambavyo vimeandikwa na wanafunzi ambao ni zao la SUA hali ambayo inaonesha ni jinsi gani wataalamu hao wanaozalishwa SUA wanaweza kufanya kazi na wakulima katika kuendeleza sekta ya kilimo nchini.

                                            

“Pia mwaka huu tumewaongezea kitu kingine kipya ambapo tunaona sio lazima wakulima waje SUA ili kupata hizo taarifa, popote ulipo mkulima, mfanyakazi na mtu mwingine yeyote yule anaweza kupata taarifa kupitia tovuti ya maktaba www.lib.sua.ac.tz/mkulima/ au kupitia  APP ya Maktaba ya Mkulima SUA kupitia Play Store ambapo mtanzania anaweza kuipakua na kuiweka katika simu yake na kutafuta kitu chochote katika maktaba yetu, hii inatusaidia kuwafikia wakulima wengi zaidi”, amesema Mkutubi huyo.


                                      

Amesema kwa kutambua kuwa watafiti wanafanya kazi katika lugha ngumu za kisayansi, Maktaba ya Taifa ya Sokoine ya Kilimo inafanya kazi ya kuzibadilisha lugha hizo za kisayansi na kuziweka katika lugha nyepesi ya Kiswahili ambayo mkulima ataweza kuielewa kwa urahisi na hivyo kufaidika na tafiti hizo.

Maonesho ya Nanenane mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo “Chagua Viongozi Bora wa Serikali za Mitaa kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi” ambapo kwa upande wa Maktaba ya Taifa ya Sokione ya Kilimo wanasema “Taarifa na maarifa ni uzalishaji bora na mapato zaidi”.

 PICHA NA TATYANA CELESTINE


 

 

Post a Comment

0 Comments