Na: Farida Mkongwe
Wananchi wanaofuga wanyama wafugwao kama paka,
mbwa, mbuzi, ng’ombe na wanyama wengine wakiwemo wanyamapori wametakiwa kufika
au kuwasiliana na wataalamu wa Hospitali ya Rufaa ya Wanyama ya Chuo Kikuu cha
Sokoine cha Kilimo (SUA) pindi wanyama wao wanapopata changamoto ya magonjwa
ili waweze kupata tiba iliyo sahihi.
Wito huo umetolewa na Profesa Mshiriki Claudius
Luziga ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uzalishaji, Maonesho na Ushauri katika
Ndaki ya Tiba ya Wanyama na Sayansi za Afya SUA wakati akizungumza na SUA
Media kuhusu huduma
zinazotolewa na Hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Wanyama iliyopo SUA katika
banda la Chuo hicho kwenye Maonesho ya Nane nane Kanda ya Mashariki
yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere mjini Morogoro.
Prof. Luziga amesema hospitali hiyo ina uwezo wa kutibu magonjwa mbalimbali yanayoshambulia wanyama wanaofugwa na kwamba inatibu magonjwa yanayosababishwa na bakteria au virusi, magonjwa yanayoshambulia mifumo ya hewa, kuvunjika na magonjwa mengine yanayowapata wanyama kwa kutumia vifaa vyenye ubora wa hali ya juu.
Amesema mbali na magonjwa
yanayoshindikana katika kliniki ndogOndogo na kupelekwa kwenye hospitali hiyo
ya Rufaa, pia wanaangalia changamoto zinazowakabili wanyama zinazotokana na
uzazi .
“Wanyama wanaofugwa ili waweze
kuwa na faida ni lazima wazaliane ndipo walete faida na ndiyo maana hata kama
kuna changamoto ya mnyama kushika mimba tunaweza kutatua kwa kuwapa dawa au
kufanya uhamilishaji kwa sababu SUA tuna mbegu zilizo bora”, amesema Prof. Luziga.
Aidha Prof. Luziga ametoa wito
kwa wananchi wanaotembelea Maonesho ya Nane nane Kanda ya Mashariki kufika
kwenye banda la SUA ili waweze kupata elimu mbalimbali pamoja na kupata ushauri
nasaha kwa mtu anayetaka kuanzisha shamba la wanyama ambapo mtu huyo atapata
elimu ya namna bora ya kufuga na kuendeleza mifugo yake.
0 Comments