Na: Farida Mkongwe
Katika kuhakikisha wakulima,
wafugaji na wavuvi wanafaidika ipasavyo na Maonesho ya Nanenane Kanda ya
Mashariki kwa mwaka 2024, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimekuja na
teknolojia mpya, tafiti na ushauri wa kitaalamu ambao utawasaidia wakulima na
wafugaji kuongeza uzalishaji wao.
Hayo yamebainishwa Agosti, 5,
2024 na Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Kujiendeleza (ICE) iliyopo SUA Dkt.
Devota Mosha wakati akizungumza na SUA Media kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na SUA katika banda lao la Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki lililopo
katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere mjini Morogoro.
Dkt. Devota amesema ICE kazi yao ni kuratibu shughuli zote za maonesho ya Nanenane na kwa mwaka huu
wamehakikisha mada zote muhimu zinazohusu wakulima na wafugaji zinapatikana ili
kukidhi matakwa ya wakulima ikiwa ni pamoja na mada zinazohusu uzalishaji bora
wa wanyama na mifugo ya aina mbalimbali ikiwemo nguruwe, kuku na samaki.
“Kwa ujumla wadau wetu wamefurahi
sana kwa namna ambavyo tumejipanga katika maonesho haya na kikubwa
kilichowafurahisha ni kuona huduma zote muhimu za kilimo na ufugaji
zinapatikana mahali hapa kwa maana kama mtu amekuja kujifunza basi inakuwa ni
rahisi kupata huduma nyingi katika eneo moja”, amesema Dkt. Devota.
Mkurugenzi huyo wa ICE ametoa
wito kwa wananchi wote wakiwemo wakulima na wafugaji kuhakikisha wanafika
katika banda hilo la SUA na wanapofika wasiwe na haraka ya kuondoka ili kupata
kujifunza na kufaidika na matunda ya tafiti zilizofanywa na watafiti bora na wabobezi
kutoka SUA.
“Wito wangu mkubwa kwa watu wanaokuja kwenye banda letu, banda la SUA lina idara nyingi naomba wanaofika watumie muda mwingi ili waweze kujifunza na kuelewa, hawatakiwi kuwa na haraka kwa sababu kila banda linatoa elimu nzuri yenye manufaa, kwa ujumla mabanda yetu yana lengo la kuboresha kilimo na kwa wafanyabiashara waweze kuwa na biashara zitakazowaongezea kipato na hivyo kukuza uchumi wao na wa Taifa kwa ujumla”, amesema Dkt. Devota
0 Comments