SUAMEDIA

Wakulima wa Uyoga watakiwa kutumia Mbegu zilizotafitiwa na SUA ili kupata mazao yenye tija

 Na: Farida Mkongwe

Wakulima wametakiwa kulima kilimo cha uyoga kwa kutumia mbegu zilizofanyiwa utafiti na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ili waweze kupata mazao yenye tija ambayo yatawaongezea kipato kwenye kaya zao.

                                  

Ushauri huo umetolewa Agosti 7, 2024  na Mwanasayansi wa Maabara kutoka Idara ya Sayansi za Viumbe Hai SUA Bw. James Mwesongo wakati akizungumza na SUA Media kwenye Maonesho ya Nane nane Kanda ya Mashariki yanayofanyika katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere mjini Morogoro.

                                

Bw. Mwesongo amesema kilimo cha uyoga ni rafiki wa mazingira na hakihitaji mtaji mkubwa wala ardhi kubwa kama ilivyo kwa mazao mengine na ni kilimo kinachotumia muda mfupi hadi kuvunwa na kwamba kitu kikubwa kinachohitajika ni kuhakikisha mkulima anatumia mbegu iliyo bora.

                                    

“Kilimo hiki kinatumia masalia ya mazao ambayo yameonekana kutokuwa na thamani kumbe yanaweza kutumika kuzalishia uyoga ambao ni chakula chenye thamani sana ambacho hata gharama yake ya mauzo ni kubwa kwa sababu kilo moja ya uyoga inauzwa kati ya Sh. 8,000/= hadi 10,000/=”, amesema Bw. Mwesongo.

                                           

Akizungumzia namna uyoga unavyolimwa Bw. Mwesongo amesema “unakusanya masalia ya mazao mbalimbali unakata vipande vidogo vidogo vya sentimeta 3 hadi 5 kisha unaloweka usiku kucha baada ya hapo unachemsha, yakishapoa unapanda mbegu zako na kushindilia kwenye mifuko hapo unapeleka sehemu ya giza kwa majuma mawili, baada ya hapo unatoa kwenye mwanga unasubiri tena majuma mawili unakuta uyoga unatoka kama hali ya hewa inakuwa nzuri”.

                                   

Amesema changamoto kubwa ya kilimo hicho  ni kuwa watu wengi hawana uelewa wa uyoga na baadhi yao wanachanganya na uyoga wa porini ana kusema una sumu jambo ambalo si kweli kwani uyoga unaopandwa ni uyoga salama kwa matumizi ya binadamu.









Post a Comment

0 Comments