Na: Farida Mkongwe
Wafugaji wa samaki wametakiwa
kutumia teknolojia mpya ya BIOFLOC ambayo ni muunganiko wa mimea midogo midogo
na bakteria ambayo huboresha ukuaji wa samaki na kudumisha ubora wa maji kwenye
bwawa la samaki na hivyo kumfanya mkulima kufuga kwa tija.
Wito huo umetolewa na Mhadhiri
Msaidizi kutoka Idara ya Sayansi ya Wanyama, Ukuzaji Viumbe Maji na Nyanda za
Malisho Mariamu Bakari wakati akizungumza na SUA Media kwenye Maonesho ya
Nanenane Kanda ya Mashariki kuhusu changamoto mbalimbali zinazowakabili
wafugaji wa samaki.
Amesema SUA wamekuja na hiyo
teknolojia iliyo bora baada ya watafiti wengi kujaribu kuangalia njia mbadala
ambayo itaweza kupunguza gharama za chakula na kudhibiti ubora wa maji ambayo
yanafugiwa samaki lakini changamoto hiyo bado imeendelea kuwepo.
“SUA tumekuja na teknolojia
nyingine ambayo ni bora zaidi inaitwa BIOFLOC, teknolojia hii inafanya kazi kwa
kuongeza wanga kwenye bwawa la samaki ambao huongeza uzalishaji wa bakteria
ambao huondoa ammonia kwenye bwawa
ambapo chembe chembe za floc ambazo
hupatikana baada ya bakteria kuchanganyika na mimea hutumika kama chakula cha
samaki”, amesema Mhadhiri huyo.
Amezitaja faida za teknolojia
hiyo kwenye ufugaji wa samaki kuwa ni kufuga samaki wengi kwenye eneo dogo
yaani zaidi ya samaki 250 kwa ujazo wa mita moja, huongeza kiwango cha kuishi,
huongeza ukuaji wa samaki na hupunguza kiwango cha chakula cha samaki.
Faida nyingine ni kuzuia magonjwa
ya samaki, huondoa kiasi cha ammonia kwenye bwawa la samaki kwani ammonia ni
moja ya vitu ambacho vinaathiri ukuaji wa samaki pamoja na kusaidia katika
suala la utunzaji wa mazingira na pia wale bakteria huwa wanakutana na vijimea
vidogo vidogo vya asili ambavyo samaki wanakula na hivyo kusaidia kupunguza
gharama za chakula.
“Wafugaji wengi wanakabiliwa na
changamoto ya kuhifadhi ubora wa maji, kukosa eneo la kufugia samaki, gharama
za chakula ni kubwa na upatikanaji wa maji ya kufugia samaki, hivyo kwa hiyo
teknolojia hii itawasaidia kwa sababu mfugaji habadilishi maji kwa miezi yote
kuanzia vifaranga hadi mavuno kama ni miezi 5 au 6 na hivyo unatunza mazingira
pia”, amesema Mhadhiri huyo.
0 Comments