Na: Winfrida Nicolaus
Wananchi wametakiwa kufika kwenye Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Kanda ya Mashariki katika Banda la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA, Kitengo cha Bustani kwa ajili ya kupata huduma za namna bora ya kulima kilimo cha mboga mboga na mazao ya bustani kisasa na kwa tija ili kujikwamua kiuchumi lakini pia kuboresha lishe ya mlaji.
Amebainisha hayo Afisa Kilimo Mwandamizi katika Ndaki ya Kilimo, Idara ya Mimea Vipando na Mazao ya Bustani SUA Bw. Godwin Rwezaula wakati akizungumza na SUAMEDIA kuhusiana na vitu ambavyo wanaionesha jamii katika maonesho hayo yanayofanyika mkoani Morogoro.
Amesema kitengo hicho cha Bustani kinahusika katika uzalishaji wa mazao ya bustani ambayo yanaweza kulimwa katika maeneo mengi ya Tanzania na kuwa na ubora mkubwa kwa kuwa yanafuata taratibu zote za kilimo cha kisasa, kilimo ambacho kitawawesha wananchi kujiongezea kipato na kuweza kuzihudumia familia zao ikiwa ni pamoja na kusomesha watoto wao.
“Tunawashauri wananchi kufika kwenye Maonesho ya 8-8 katika Banda la SUA Kitengo cha Bustani kwa ajili ya kupata huduma za namna bora ya kufanya kilimo cha kisasa na cha tija kwenye maisha yao ya kila siku kwa kuwa watapata elimu ya namna ya kuzalisha kwa viwango na ubora stahiki lakini pia kuona vile vitu ambayo tumezalisha na vimeleta tija ”, amesema Bw. Rwezaula
Bw. Rwezaula ameongeza kuwa wanazo mbegu zilizofanyiwa utafiti na SUA ambazo zimelenga katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi lakini pia zinazozingatia lishe pamoja na ukinzani na magonjwa hivyo mazao yatokanayo na mbegu hizo ni yenye ubora na tija ambayo yatamsaidia mkulima kiuchumi lakini pia kuboresha lishe .
Kwa upande wake Edgna Wella Muhitimu Shahada ya Kilimo cha Bustani SUA amesema wameleta miche ya matunda ya aina mbalimbali yenye ubora wa hali ya juu kwa kuwa imezalishwa kitaalam ikiwemo miche ya embe, parachichi za aina tofauti, machungwa, machenza, mapera, mastafeli, midarasini, ndimu pamoja na limao.
“Mwananchi akifika hapa kwenye banda la SUA ana uhakika wa kupata miche bora ambayo itampatia matunda yaliyo bora na itakuwa inadumu kwa muda mrefu kwenye shamba lake kwa ubora ule ule”, amesema Muhitimu huyo.
Naye Simon Mayonga ambaye ni Bwana Shamba katika Idara Mimea Vipando na Mazao ya Bustani amesema watu wanapoenda kwenye banda lao pamoja na mambo mengi ambayo wanaweza kujifunza moja ya kitu cha msingi sana ambacho watajifunza ni Kilimo Biashara.
“Kitu wanachotakiwa kukielewa ni kuacha kuchukulia kilimo cha mboga mboga na bustani kama kitu cha kawaida kwa kuwa endapo mkulima akitia shime na kuweka kipato chake kwenye uzalishaji wa kilimo hiki licha ya kupata lishe bora ataongeza kipato kitakacho muwezesha kuendesha maisha yake”, amesema Bw. Mayonga
0 Comments