Na: Winfrida Nicolaus
Wakazi wa Mkoa wa Morogoro na maeneo ya jirani wametakiwa kufika kwenye banda la Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) katika Maonesho ya Nanenane Kanda ya
Mashariki ili kupata elimu na ushauri wa kitaalamu juu ya ulaji sahihi ambao
utawaweka mbali na magonjwa.
Amebainisha
hayo Dkt. Zahra Majiri Mhadhiri kutoka SUA, Idara ya Sayansi ya Lishe na Stadi
za Mlaji wakati akizungumza na SUA Media katika banda la Chuo hicho kwenye Maonesho hayo yanayoendelea katika
viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere mjini Morogoro.
Amesema Lishe
bora ina faida nyingi mwilini kwa kuwa inakufanya uweze kuwa na uwezo wa kuwa
na afya bora, uwezo wa kufikiri vizuri na kufanya kazi kwa ufasaha hata
kupelekea uwezo wa uzalishaji wenye tija.
“Unapokosa
Lishe bora ina maana utakosa nguvu, uwezo wa kufikiri na hata uzalishaji wako
utakuwa mdogo, vile vile inaweza kukufikisha kwenye magonjwa mbalimbali hasa
yale sugu yasiyoambukiza ikiwemo magonjwa ya moyo, presha na kisukari”, amesema
Dkt. Zahra.
Aidha Dkt.
Zahra amesema bidhaa yao kuu kwenye maonesho hayo ni kutoa elimu ikiwemo
makundi ya vyakula vile vile kiasi
ambacho mtu anahitajika kukipata au kula kwa siku ili afya yake iwe salama
lakini pia wanahimiza ufanyaji wa mazoezi kwa ajili ya utunzaji wa afya ya
mlaji na kuimarisha mwili.
Ameongeza
kuwa licha ya kutoa elimu wanazo pia bidhaa za lishe ikiwemo unga wa uji
uliotengenezwa kwa kuzingatia mahitaji ya muhusika lakini pia makundi ya
chakula vile vile kuna bidhaa ya biskuti ambayo ipo tofauti na ile ya mtaani inayotumia
ngano pekeeambapo wameitengeneza biskuti hiyo kwa kuiongezea thamani kwa kutumia
viazi lishe pamoja na mbaazi.
“Sasa hivi
tunahamasisha lishe bora kwa watoto kwa kuwa watoto walio wengi imeonekana wana
upungufu wa madini ya chuma mwilini vile vile upungufu wa Vitamini A hivyo
tumeiongezea thamani biskuti hiyo kwa kuweka viazi lishe na mbaazi ambapo itawasaidia
kukutana na madini ya chuma, vitamini mbalimbali na zinki kwa wingi zaidi
watakapotumia biskuti hizo”, amesema Dkt. Zahra.
0 Comments