SUAMEDIA

SUA yatoa elimu ya usindikaji na uchakataji wa mazao ya kilimo

 

Na: Winfrida Nicolaus

Idara ya Teknolojia ya Chakula na Uchakataji wa Mazao ya Shambani iliyopo katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA inatoa elimu kwa wakulima na jamii kwa ujumla juu ya namna nzuri za kufanya usindikaji na uchakataji wa mazao ya shamba kuwa katika bidhaa zenye thamani kibiashara.

                                

Amebainisha hayo Bw. Tamambele Masinga Fundi Sanifu kutoka Maabara ya Chakula Idara ya Sayansi ya Chakula na Uchakataji  wa Mazao SUA wakati akizungumza na SUA Media katika banda la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwenye Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yanayofanyika katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere mjini Morogoro.

                                

Amesema wapo katika maonesho hayo kwa lengo la kutoa elimu kwa wakulima hasa ambao wanahusika na mazao ya shamba ili wajifunze namna nzuri ya kubadilisha mazao ya shamba kuwa bidhaa ambazo zinakuwa na kiwango kirefu cha muda.

“Kwa maana hiyo sasa kile tunachokifanya tunatoa katika mazao ya shamba na kuja kuwa bidhaa ambayo ina thamani zaidi na hii ni kuhakikisha tunapata uhakika wa uwepo wa Chakula ambacho ni salama wakati wote kwa mwaka mzima, chakula ambacho kinaweza kuwa faida kubwa kwa watumiaji wa aina mbalimbali”, amesema Masinga.

                                

Aidha Bw. Masinga amesema anawahamasisha wananchi kupata mafunzo mbalimbali ya muda mfupi kwa faida yao wenyewe kwa sababu wale ambao wanapata ujuzi kama wa uchakataji wa mazao kama vile matunda kwa ajili ya Juisi, mvinyo, unga wa usindikaji wa mboga mboga itawasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza uharibifu wa mazao ya shambani ambayo yangeweza kuharibika kama yangeachwa bila kubadilishwa au kuyaongezea thamani.

Ameongeza kuwa wamekuja na bidhaa mbalimbali ambazo zimetengezwa na wanafunzi kupitia usimamizi mzuri wa Wataalam wa Maabara na wanazionesha katika maonesho hayo ikiwemo Juisi  ambayo imetokana na matunda ambayo hayapo kwenye msimu, unga wa Lishe pamoja na biskuti zilizotengenezwa kwa viazi lishe, njugu mawe na mlonge.

 










Post a Comment

0 Comments