Na: Farida Mkongwe
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka wahitimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kuitumia elimu bora ya kilimo wanayoipata chuoni hapo kuongeza uzalishaji katika sekta ya kilimo na kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili wakulima nchini.
Rais Samia ametoa kauli hiyo Agosti 6, 2024 wakati akizungumza na wanajumuiya ya SUA baada ya kuzindua Jengo Mtambuka la Mafunzo liliopo SUA Kampasi ya Edward Moringe na kukipongeza Chuo hicho kwa kutoa elimu yenye ubora wa hali ya juu kwa wanafunzi wake na kusema kuwa anaamini matunda ya wahitimu hao yanaonekana wazi wazi kwa wakulima.
“Matarajio yangu kwa vijana mnaotoka SUA baada ya sera na mipango yote inayowekwa na SUA katika kutengeneza nguvu kazi ya Tanzania, ni matumaini yangu kama mnavyotengenezwa hapa hamtakuja kusumbua sana katika ajira, bila shaka wapo tutakao wameza kwenye ajira hapa hapa chuoni, kwenye vyuo mbalimbali vya mifugo, vyuo vya kilimo na sekta nyinginezo ambavyo vyote hivyo vinatumika kwa ajili ya kuwasaidia wakulima wetu” amesema Mhe. Rais Samia.
Amesema kwa kiasi kikubwa vijana hao wanaohitimu SUA watakwenda kuungana kwenye Programu kubwa ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) , na kwamba Serikali itajitahidi kutafuta fedha ili kuwapa nguvu wakiwa kwenye Programu hiyo kwa lengo la kukuza ajira lakini pia kukuza Sera ya kilimo biashara.
“Ombi langu kwa wanafunzi wanaohitimu hapa SUA ni kwenda huko kwenye Programu yetu ya BBT, bahati nzuri Waziri Bashe yupo hapa na sasa hivi najua kashavua kofia anakuna kichwa kufikiria namna atakavyoweza kuwaingiza huko na fedha atatoa wapi lakini Mungu atatufungulia njia tutaweza”, amesema Mhe. Rais Samia.
0 Comments