Na: Winfrida Nicolaus
Wananchi
wa Mkoa wa Morogoro na mikoa ya jirani wakiwemo wahitimu wa kidato cha nne na
sita wanakaribishwa kutembelea Banda la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)
lililopo katika viwanja vya Maonesho ya
Nanenane Kanda ya Mashariki ili kupata elimu juu ya vigezo vya kujiunga na programu
za Shahada mbalimbali chuoni hapo, jinsi ya kujisajili pamoja na kupata
usaidizi wa moja kwa moja wa kujiunga na Chuo hicho.
Amebainisha
hayo Afisa Udahili wa Shahada za Awali SUA Bi. Grace Kihombo Agosti 3, 2024
wakati akizungumza na SUAMEDIA kwenye Maonesho hayo ambapo amesema dirisha la
udahili lipo wazi tangu Julai 15, 2024
na litafungwa Agosti 10, 2024 hivyo amewataka
wadau wote wenye sifa za kujiunga na Chuo chao kuwatembelea ili kupata elimu na usaidizi wa
kujiunga na Chuo hicho.
“Wakija
hapa watapata Elimu kuhusu Shahada tunazozitoa na vigezo vyake, tuna Shahada
mbalimbali ambazo SUA tunazitoa ndani ya
Kurugenzi ya Shahada za Awali , tunazo Shahada za Kilimo, Misitu, Ufugaji wa
Nyuki vile vile ufugaji wa wanyama hivyo
wakija hapa watapata kuelewa sifa za kujiunga na Shahada hizo”, amesema Bi.
Grace.
Aidha Afisa
Udahili huyo amesema imekuwa ikieleweka SUA ni kwa ajili ya masomo ya sayansi pekee
lakini pia wanatoa Shahada za sanaa
hivyo ametoa rai kwa wananchi na wadau wote ambao wamesoma masomo hayo kujiunga
na SUA ili kupata elimu bora, vile vile kwa wale ambao wamemaliza kidato cha
nne wanaweza kusoma Astashahada mbalimbali zilizopo chuoni hapo.
Kwa
upande wake Bi. Stellah Jacob Afisa Udahili katika Kurugenzi ya Uzamili,
Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalam SUA amesema wanatoa
ushauri wa kitaalama kuhusiana na kozi wanazozitoa kwenye Kurugenzi yao na
ushauri kwenye masuala ya Tafiti na Teknolojia mbalimbali zinazozalishwa chuoni
hapo.
Ameongeza
kuwa dirisha la udahili limefunguliwa tangu Juni 6, 2024 kwa upande wa watu wa
shahada za Uzamili (MASTERS) na zoezi hilo litakamilika mwishoni mwa mwezi Oktoba
vile vile kwa upande wa watu wa Uzamivu (PHD) hasa zile za course work zitakamilika
mwezi Novemba hivyo ni muhimu kufanya udahili kwa kuzingatia muda uliotolewa.
Maonesho
hayo ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi kwa mwaka huu 2024 yamebeba kauli mbiu isemayo
“Chagua Viongozi Bora wa Serikali za Mitaa kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo,
Mifugo na Uvuvi”.
0 Comments