Na: Farida Mkongwe
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Shule Kuu ya Elimu kimesema kinatekeleza kwa vitendo program tatu ambazo wanatakiwa kuzitekeleza kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Mafiga kama ilivyoelekezwa na Serikali kupitia Mitaala ya Elimu ya Amali kwa mujibu wa Mitaala Mipya kwa Elimu ya shule za msingi na sekondari.
Hayo yamebainishwa na Mratibu wa Shule ya Sekondari Mafiga Dkt. Benedicto Msangya wakati akizungumza na SUA Media kwenye Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yanayofanyika mjini Morogoro.
Dkt. Msangya amesema shule ya sekondari Mafiga ni shule ya mazoezi kwa Shule Kuu ya Elimu ambayo wanaitumia kwa ajili ya wanafunzi wao kuweza kufanya elimu kwa vitendo yaani kile ambacho wanajifunza wakiwa darasani wanakwenda kukifanyia kazi kwa vitendo katika shule hiyo ya sekondari Mafiga.
“Serikali kupitia mitaala ya Elimu ya Awali imetuletea program tatu pale Mafiga ambazo zipo kwenye Mkondo wa Awali, program hizo ni uzalishaji wa mazao, uzalishaji wa wanyama na kilimo cha bustani ambapo Serikali imeshatuletea wanafunzi pale Mafiga katika program zote tatu”, amesema Dkt. Msangya.
Amesema kwa sababu hii program ni mpya wanafunzi katika hatua ya awali wataweza kupata mafunzo kwa vitendo kule SUA ambapo itawasaidia watakapomaliza shule ya sekondari waweze kujiajiri na wale watakao kwenda kwenye ngazi ya juu waweze kuwa wanafunzi bora na hivyo kuweza kulitumikia taifa.
Lengo kuu ya Elimu ya Amali ni kukuza ujuzi unaoweza kutumika moja kwa moja katika mazingira halisi ya kazi au maisha ambapo kwenye kilimo na ufugaji inachangia sana katika mazoezi ya ubunifu na utafiti wa mazao, vitalu, wanyama na kutengeneza miundombinu ya kilimo, matumizi ya zana na mashine mbalimbali za kilimo na mbinu za uokoaji mazao, mifugo na miche.
0 Comments