SUAMEDIA

Kitumieni vizuri Chuo Kikuu cha SUA ili kuwa na kilimo chenye tija- Mhe. Pinda

 

Na: Farida Mkongwe

Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Kayanza Pinda  amewataka viongozi wa Kanda ya Mashariki na wananchi kwa ujumla kuvitumia vizuri Vyuo Vikuu kikiwemo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Vyuo vya Kati na Vyuo vingine vya ngazi ya chini vilivyopo mkoani humo katika kuendeleza Sekta ya kilimo nchini.

                                    

Mhe. Pinda ametoa kauli hiyo Agosti 8, 2024 wakati akifunga Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere mjini Morogoro na kusema kuwa Kanda hiyo ina bahati kubwa ya kuwa na vyuo vikuu vingi na kwamba kinachotakiwa ni kujipanga ili kuweza kuzitumia rasilimali zilizopo katika vyuo hivyo.

                                        

“Bahati nzuri Kanda hii mna bahati kubwa sana, mna vyuo vikuu, vyuo vya kati na vyuo vingine vya ngazi ya chini, kubwa zaidi ndani yake ni uwepo wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, hawa ndiyo wanaibua vichwa vinavyokuja baadaye kusimamia shughuli za kilimo, uvuvi na ufugaji, kwenu ni tuzo kubwa, kinachotakiwa ni kutafuta namna ya kuzitumia tuzo hizo ili zitupeleke mbele ”, amesema Mhe. Pinda

Kabla ya kufunga Maonesho hayo Mhe, Pinda alitembelea mabanda mbalimbali likiwemo banda la SUA na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na banda hilo ikiwa ni pamoja na tafiti na teknolojia ambazo zinaongeza tija katika uzalishaji wa mifugo na mazao ya kilimo.

                                

Katika Maonesho ya Nanenane ya mwaka huu Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeibuka mshindi wa pili kwa upande wa Taasisi za Mafunzo na Utafiti, mshindi wa kwanza ni Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) na mshindi wa tatu ni  Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA).

Akizungumzia ushindi huo Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Kujiendeleza (ICE) SUA Dkt. Devota Mosha amewashukuru washiriki wote wa Maonesho ya Nanenane kwa banda la SUA na kusema kuwa wanajipanga ili mwakani wawe washindi wa kwanza kama ilivyo kawaida yao.

“Nichukue nafasi hii kuwashukuru washiriki wote kwa sababu tumekuwa na mambo mengi mapya na watu wamefurahia sana labda changamoto kubwa ambayo tumeiona ni wenzetu TARI kuwa na vipando vingi zaidi yetu, niwaombe washiriki wote wa SUA tuimarishe vipando vyetu ili mwakani tuendelee kushinda nafasi ya kwanza kama ilivyokuwa kwa miaka ya nyuma”, amesema Dkt. Devota.

       

       


           

           

           

           

            



             


             


             PICHA NA  TATYANA CELESTINE

Post a Comment

0 Comments