SUAMEDIA

SUA yajivunia ushirikiano na Chuo Kikuu cha Kilimo cha China

 

Na: George Alexander

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kinaendelea kujivunia ushirikiano wake na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Shenyang cha nchini China ulioanza mwaka 2017.



Akizungumza na SUA Media Agosti 12, 2024  baada ya kuwapokea na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Chuo cha Kilimo cha Shenyang pamoja na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha SUA Prof. Raphael Chibunda,  Prof. Japhet Kashaigili ambaye ni Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, na Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalam amesema kuwa wamekutana kwa lengo la kuyapitia makubaliano waliyoingia mwaka 2017 na namna gani ya kuyaendeleza.

Amesema moja kati ya makubaliano hayo ilikuwa ni kubadilishana wataalamu pamoja na wanafunzi, na kuwa Chuo Kikuu cha SUA kimeshanufaika na mashirikiano hayo na kuwa kuna idadi ya madaktari ambao wameshakwenda kusoma katika Chuo hicho na sasa wanaendelea kufanya shughuli zao hapa chuoni.




Pia Prof. Kashaigili amesema katika kikao hicho wamejadili namna ya kuyaendeleza makubaliano hayo na kufanya zaidi ya hapo kwa kuanzisha programu maalumu ya kibiashara ya kimataifa ya kilimo na pia kupeleka walimu wengi zaidi kutoka SUA kwenda China na wataalamu wa Chuo hicho kwenda SUA.

Aidha Prof. Kashaigili amebainisha kuwa uendelevu huo wa makubaliano na urafiki kati ya vyuo hivyo viwili utaleta manufaa kwa Chuo Kikuu cha SUA pamoja na taifa kwa ujumla kwa maana utalaamu huo ukija hautaishia Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo.

“Maendeleo haya ni endelevu na yana faida kwa Chuo chetu na kwa Nchi kwa ujumla kwa maana utaalamu ukija hauishii tu kwa Chuo chetu bali utasambaa kwa taifa zima”, amesema Prof. Kashaigili

Naye Makamu wa Rais wa Chuo hicho cha Kilimo cha Shenyag Prof. Li Bin amesema kuwa lengo lao lililowaleta ni kupitia makubaliano waliyoingia awali na pia kuanzisha makubaliano mapya.





Post a Comment

0 Comments