SUAMEDIA

Wanafunzi wa Wilbalda Sekondari yafanya Ziara SUA kujifunza kilimo kwa vitendo

 

Na: AYOUB MWIGUNE

Wanafunzi wa kidato cha tatu wanaosoma somo la kilimo kutoka Shule ya Sekondari Wilbalda iliyopo Kabuku mkoani Tanga wametembelea Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na kupata fursa ya kuona namna kilimo kinavyofanyika kwa vitendo kupitia somo la kilimo ambalo linafundishwa shuleni kwao pamoja na kukuza ufahamu wao juu ya shughuli zinazofanywa na Chuo hicho .

                            

Hayo  yameelezwa  na Venance Peter   ambaye ni  Mwalimu kutoka shule hiyo wakati akizungumza na SUAMEDIA kuhusiana na lengo la kutembelea SUA kwa wanafunzi wanaosoma somo hilo.

Mwl. Peter amesema kimsingi shule yao inafundisha somo la kilimo hivyo wameona ni vyema kwa wanafunzi hao kuweza kutembelea Chuo Kikuu cha SUA kwa ajili ya kuweza kujifunza kwa vitendo kwa wanafunzi hao kwani SUA ina vifaa vya kisasa ambavyo  kwa taasisi nyingine hawana, mfano mashine ya kukamua maziwa ya ng’ombe pamoja  na kuwa na wataalam waliobobea katika kilimo.

 “Tumeweza kujifunza ufugaji wa Sungura, Nguruwe, Kuku pamoja na Ng’ombe kuanzia kuzaliwa kwake mpaka ukuaji wake, vile vile tumepata nafasi ya kujifunza uzalishaji wa samaki, samaki anapotaga mayai mpaka hatua ya mwisho.” amesema mwl. Peter.

                            

Aidha Mwl. Peter amesema SUA imewapa wanafunzi wao mwangaza na kurejea shuleni kwao Wilbalda tayari wakiwa wamejaa ujuzi na maarifa kuhusu somo la kilimo na anaamini wanafunzi hao wataenda kuwa mabalozi wazuri kuhusiana na Chuo hicho.

Vile vile Mwl. Peter ametoa wito kwa shule nyingine nchini ambazo zinafundisha somo la kilimo kuweza kukitumia Chuo Kikuu cha SUA  katika kukuza uelewa kwa walimu wa masomo hayo pamoja na wanafunzi katika kujifunza kwa vitendo  ambapo wao wameweza kunufaika kwa kwa kiasi kikubwa hali itakayowasaidia katika kukuza shughuli zao za kilimo.

                            

Kwa upande wake Epiphania Sembeka ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu kutoka shule hiyo  amesema wamejifunza mambo mbalimbali katika ufugaji sambamba na namna ya kuweza kuikinga mifugo na magonjwa mbalimbali hivyo kupitia  SUA amepata mwangaza wa kile wanachojifunza darasani ambapo wameongeza maarifa ya kutosha hivyo ametoa rai kwa wanafunzi wenzake kutunza maarifa waliyoweza kuyapokea chuoni hapo .

“Nawashukuru SUA kwa elimu ambayo wametupatia itaweza kutusaidia kwa baadaye tuweze kuwa watu wakubwa katika kilimo ambapo tutajenga uchumi wa taifa.” amesema Seberua Maganga mwanafunzi wa shule hiyo.










Post a Comment

0 Comments