SUAMEDIA

SUA yaja na mbinu mpya ya kuzalisha mpunga wenye tija kwa kutumia Azolla

Na: Farida Mkongwe

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimekuja na mbinu mpya ya uzalishaji mpunga kwa kutumia zao la Azolla ambalo licha ya kuwa na virutubisho pamoja kutumika kama mbolea ya asili pia linasaidia kupunguza ukuaji wa magugu ambayo yanaweza kugombania virutubisho kwenye mpunga na kupunguza mavuno ya zao hilo.

                                        

Hayo yamebainishwa Agosti 2, 2024 na Mhadhiri Msaidizi wa Idara ya Sayansi za Udongo na Jiolojia Ndaki ya Kilimo Dkt. Monica Nakei kutoka SUA wakati akizungumza na SUA Media katika banda la Chuo hicho kwenye Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere mjini Morogoro.

Dkt. Nakei amesema zao la Azola kwa kawaida wengi wamezoea linatumika katika kilimo au ufugaji samaki lakini SUA kupitia Idara hiyo wamefanya utafiti na kubaini kuwa Azolla inasaidia kupunguza upotevu wa maji katika skimu za umwagiliaji na hivyo kumfanya mkulima aweze kulima kwa tija kwa sababu zao la mpunga linahitaji kuwepo kwa maji ya kutosha.

“Sasa tumekuja na mbinu mpya ya uzalishaji wa mpunga, tunajua Azola inapenda sana sehemu yenye maji kama bwawa na mpunga unapenda sana maji sasa hii Azolla kwa kusaidiana na viumbe wengine kwenye udongo ina uwezo wa kuchukua nitrojeni iliyopo hewani ikaleta kule kwenye maji ikachukuliwa na mmea ”, amesema Dkt. Nakei.

“Azolla yenyewe pia inatumika kama mbolea ya asili kwa sababu ni zao linalokuwa haraka kwa hiyo inapokuwa haraka na baadaye ikioza inarudisha tena virutubisho kwenye mpunga na hiyo kuufanya mpunga kuwa na afya nzuri na hivyo mkulima kupata mazao yenye tija”, amefafanua Dkt. Nakei

Amesema wamefanya tafiti nyingi ikiwemo ya kutengeneza mbolea inayotokana na viumbehai visivyoonekana kwa macho jamii ya bakteria waliopo kwenye  udongo ambapo viumbehai hao humeng’enya fosforasi ambayo ipo kwenye udongo ambayo haipatikani kwa ajili ya matumizi ya mimea.

“Udongo unakutana na changamoto mbalimbali kama chumvu chumvi au tindikali kukiwa na tindikali haya madini ya fosforasi yanashikiliwa na madini mengine kama aluminiam na chuma katika udongo kwa hiyo yanakuwa hayachukuliwi na mmea, lakini udongo ukiwa na chumvi nyingi yanashikiliwa na madini yanayoitwa calicium hivyo hii fosforasi inakuwa haichukuliwi na mimea sasa hawa bakteria wakishaimeng’enya inakuwa kwenye udongo na hivyo kuchukuliwa na mimea”, amesema Dkt. Nakei

                             




Post a Comment

0 Comments