SUAMEDIA

Serikali kuendelea kuunga mkono jitihada za SUA za kuongeza tija katika kilimo

 

Na: Farida Mkongwe

Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za kuendeleza kilimo zinazofanywa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)  katika utekelezaji wa majukumu yake ikizingatia dhamira ya Chuo hicho ya kuongeza tija katika uzalishaji wa kilimo.

                            

Rais Samia ametoa kauli hiyo Agosti 6, 2024 wakati akizungumza na Wanajumuiya wa SUA baada ya kuzindua Jengo Mtambuka la Mafunzo na kutoa pongezi maalum kwa Menejimenti ya SUA kwa namna inavyosimamia miradi ya Chuo hicho na kujiongezea mapato ya ndani.

“Hapa sasa nataka nitoe pongezi maalum nilimsikiliza Mwenyekiti wa Baraza la Chuo akisema kuhusu miradi yote ambayo inatekelezwa na SUA katika maeneo mbalimbali na amesema miradi hii pia ni vyanzo vya mapato kwa SUA, hongereni sana katika hilo”

“Lakini pia mmesema  kuna vikundi 47 mlivyovitayarisha ambavyo mmewafundisha mambo mbalimbali wenyewe wanazalisha halafu mkawa mnawapa na tender wa-supply kwenye Chuo, hili ni jambo zuri sana hongereni sana kwa sababu mmewasomesha, mmewafundisha mkatengeneza na ajira, hili ni jambo la kutiliwa mfano kwenye vyuo vingine kwamba wafuate mtindo huo, hongereni sana sana”, amepongeza Mhe. Rais Samia.

                                

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Mhe. Jaji Mohamed Chande Othman amesema katika kuitikia wito wa Serikali wa kuboresha elimu, ujuzi na kuwajengea wanafunzi umahiri wa stadi za maisha, Baraza la Chuo hicho limeendelea kuboresha mafunzo kwa vitendo kwa kuongeza ujuzi kwa wahitimu.

Amesema Baraza la Chuo linaendelea kukihimiza Chuo na Menejimenti kuboresha Mashamba Darasa, Karakana za Uhandisi na Maabara za Misitu ya Mafunzo ili kutoa fursa kwa wanafunzi kupata mafunzo kwa vitendo ili waweze kuongeza maarifa, ujuzi na umahiri.

                            

“Baraza limeendelea kukisimamia Chuo katika utekelezaji wa mikakati ya uzalishaji wa mapato ya ndani ambapo Chuo kinaendelea kuimarisha mikakati hiyo kwa kuongeza uzalishaji wa mapato katika vitengo vyake vya ndani ili kusaidia utekelezaji wa majukumu ya Chuo hiki”, amesema Mwenyekiti huyo wa Baraza la Chuo.









Post a Comment

0 Comments