Na: Farida Mkongwe
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
(SUA) kimeendela kutoa elimu kwa wanafunzi wa Chuo hicho lakini pia kwa
wakufunzi wa vyuo vidogo, vya kati na vyuo vikuu huku ikiwekea mkazo elimu ya
vitendo ili kuwawezesha wahitimu kuwa na ujuzi utakaowawezesha kujiajiri.
Hayo yamebainishwa na Dkt. Hamidu
Hassan Khalfan, Mratibu Mkuu wa Shughuli shirikishi za Huduma ambazo SUA
kupitia Shule Kuu ya Elimu inazitoa kwa jamii na taasisi mbalimbali
zinazoizunguka SUA wakati akizungumza na SUA Media kwenye Maonesho ya Nanenane Kanda
ya Mashariki mjini Morogoro.
Dkt. Hamidu amesema Wakufunzi wa
vyuo lakini pia walimu wa shule za msingi na sekondari wanatakiwa kufundisha
kwa mujibu wa mtaala mpya ambao unawataka kufundisha Elimu ya Amali ambayo
inahusiana na mazoezi ya vitendo na ujuzi wa moja kwa moja.
“Hii tafsiri yake ni kwamba
inaendana na Serikali kwa sasa na badiliko la mitaala ambapo Serikali inatilia
mkazo Elimu ya Amali inayojikita katika maendeleo ya uwezo wa kiufundi na
kitaaluma kupitia mazoezi na matumizi ya vifaa au mbinu maalum ambayo
inapelekea wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne au sita au darasa la saba kila
mmoja awe na uwezo wa kujiajiri”, amesema Dkt. Hamidu
Amesema katika maonesho hayo ya
Nanenane kitu kikubwa wanachokielezea kwenye banda lao ni jinsi walimu watakavyowatengeneza
wanafunzi ili wawe wabunifu kwa mujibu wa Elimu ya Mkondo wa Amali ambayo
wameipata hivyo walimu wanapoenda kufundisha maana yake waende na nyenzo za
kufundishia kwa vitendo.
“Pia inawezekana kabisa
anayefundisha au kufundishwa yupo mbali hivyo tumeandaa Application ambayo inaitwa Bright
Academy E learning system Architecture, hii
inapatikana kwenye play store ya simu
yako, kwa kutumia APP hii mtu anaweza
kupata elimu ya kitu chochote anachokitaka au maelezo mfano kuhusu mifugo,
ujenzi na mengine mengi akaelekezwa na kile chuo alichotoka au mwalimu
aliyekuwa akimfundisha akiwa yupo field
kwa njia ya mtandao”, amesema Dkt. Hamidu
0 Comments