Na: Farida Mkongwe
Wakulima wameshauriwa kutumia
teknolojia ya kisasa ya kuwadhibiti panya waharibifu mashambani kwa kutumia
njia ya kibaolojia ambayo inahusisha matumizi ya Bundi katika kudhibiti panya
hao ambao wanaharibu mazao.
Ushauri huo umetolewa Agosti 4,
na Mtafiti Msaidizi Teclamageni Mayeji kutoka Taasisi ya Kudhibiti Viumbe Hai
Waharibifu katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wakati akizungumza na
SUA Media kwenye Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki kuhusu teknolojia ya
matumizi ya Bundi inavyowasaidia wakulima kuwakomboa na panya waharibifu wa
mashambani,
Amesema bundi huyo ana uwezo wa
kula panya zaidi ya 12 kwa usiku mmoja hivyo hakuna sababu ya kumchukia na
kuwataka wale wote wenye dhana potofu na kumuona bundi kama mnyama mbaya mwenye
kuleta mikosi kuachana na dhana hiyo badala yake wamuone kuwa ni rafiki mzuri
wa wakulima kwani ana uwezo mkubwa wa kuwakomboa wakulima dhidi ya panya
waharibifu wa mashambani.
“Sisi tunamuita bundi kama rafiki
wa mkulima, jinsi ya kumpata utatakiwa kuandaa kihota chako vizuri kwa ajili ya kumvutia
bundi, hapo bundi ana uwezo wa kuja na kuingia katika kihota hicho na kuweza
kukaa na kudhibiti panya waliopo katika shamba lako, hivyo hatuna sababu ya
kumuogopa wala kumuhofia”, amesema Mtafiti huyo.
Amesema ni vizuri kutumia
teknolojia hiyo ambayo kazi yake ni kuandaa kihota tu ambacho kitamuwezesha
bundi huyo kukaa na kwamba teknolojia hiyo ina faida zaidi ukilinganisha na
matumizi ya sumu za kuua panya ambazo usipofuata maelekezo vizuri unaweza
kuleta madhara katika afya za binadamu.
0 Comments