SUAMEDIA

SUA yaendelea kusifika katika kutoa elimu bora pamoja na tafiti zenye tija

 

Na:Tatyana Celestine     

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kimeendelea kusifika katika kutoa elimu bora pamoja na Tafiti zenye tija katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi katika ukanda wa Mashariki ambapo wananchi wameaswa kutumia fursa ya kuwepo kwa taasisi zinazosifika kufanya vizuri katika utafiti nchini ili kupata elimu bora katika shughuli zao za mifugo, kilimo na uvuvi kama agenda ya Rais Samia Suluhu Hassan ya 10/30 kuhakikisha  sekta hizo zinaongeza kipato cha taifa kwa asilimia 30.                                                                                            

                        

Hayo yamebanishwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Buriani wakati akifungua Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki katika viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mkoani Morogoro Agosti 2, 2024 yaliyobeba kauli mbiu isemayo “Chagua Viongozi Bora wa Serikali za Mitaa kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi”.

Dkt. Buriani  amekipongeza Chuo hicho kwa kutumia mabadiliko ya tabianchi kama fursa kwa kufanya tafiti mbalimbali zinazosaidia kuendeleza kilimo nchini na kuwataka wakulima na wafugaji kutumia fursa ya maonesho hayo kwa kutembelea SUA kujifunza vitu vipya kama nyasi za malisho, teknolojia ya upimaji wa udongo, miundombinu ya umwagiliaji kwani nchi haijaweza kutumia fursa kikamilifu kutokana na mabadiliko ya tabianchi ambayo husababisha ukame, mafuriko na kuongezeka kwa joto hivyo ni vema kushirikiana na watafiti hao kufanya kilimo, mifugo na uvuvi kwa tija.

Aidha amewapongeza wakulima na wavuvi ambao wamejitoa kushiriki Maonesho ya Nane Nane mwaka huu na kusema kuwa ushiriki wao utasaidia kuongeza ujuzi, uwezo na mawazo tofauti kutokana na kukutana na wadau wengine kupitia maonesho hayo kama lengo lake la kutoa elimu na kuongeza wafugaji na wavuvi na wadau wengine katika mnyororo wa thamani

Kabla ya kufungua rasmi maonesho hayo, Dkt. Buriani  alitembelea mabanda mbalimbali likiwemo Banda la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) lililopo katika viwanja vya Maonesho ya Nane nane Kanda ya Mashariki na kujionea teknolojia mbalimbali zinazozalishwa na Chuo hicho.

Akiwa katika banda hilo alikaribishwa na viongozi mbalimbali wa SUA wakiongozwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam, Prof. Maulid Mwatawala ambaye alitoa maelezo kuhusu teknolojia mbalimbali zilizopo katika banda hilo.

 









Post a Comment

0 Comments