Na: Ayoub Mwigune
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara ya kikazi ya
siku tano mkoani Morogoro kuanzia tarehe 2 hadi 7 Agosti 2024, kwa lengo la
kutembelea na kukagua miradi ya
maendeleo sambamba na kuzungumza na
wakazi wa mkoa huo.
Hayo yameelezwa Julai 30, 2024 na Mkuu wa mkoa wa Morogoro Adam Malima wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu ziara hiyo.
Malima amesema Rais Samia ataanzia ziara yake katika wilaya
ya Gairo ambapo atakagua miradi mbalimbali sambamba na kuzungumza na wananchi
wa wilaya hiyo ambapo Agosti 7, 2024 atazungumza na wakazi wa Morogoro katika
uwanja wa Jamhuri uliopo Manispaa ya Morogoro.
Mkuu huyo wa mkoa amewaomba wakazi wa
Morogoro kujitokeza kwa wingi kumpokea na kumsikiliza Mhe. Rais kwani ujio wake
katika mkoani humo ni utekezaji kwa vitendo wa namna ambavyo Serikali ya Awamu ya
Sita ilivyoweza kuwekeza katika miradi mbalimbali ya kimaendeleo kama maji, elimu
na usafirishaji.
Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa
Mkoa huo akiwemo Bw. Shaban Ramadhan na Flavian Nofred wamesema ziara ya Mhe. Samia
itatoa mwangaza katika sekta ya kilimo
kwani mkoa wa Morogoro umekuwa ukifanya vizuri katika sekta hiyo.
Wamesema kuwa ziara hiyo ya Rais
Samia itawapa nafasi wakulima kuweza kusikia malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita
katika kilimo huku wakitoa wito kwa wakazi wa Morogoro kujitokeza kwa wingi ili
kumsikiliza Mhe. Rais.
0 Comments