Na: Farida Mkongwe
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amezindua Jengo Mtambuka la Mafunzo
liliopo katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na kuridhia ombi
lililotolewa na Mkuu wa Chuo hicho Mhe. Jaji Joseph Sinde Warioba la kutaka Jengo
hilo liitwe jina la Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza wakati akitoa salaam
kwa wanajumuiya wa SUA katika uzinduzi huo, Mhe. Rais amesema amekubali ombi
hilo lakini akatoa ombi la kutaka jengo lingine linalojengwa na Chuo hicho
litakapokamilika basi lipewe jina la Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael
Chibunda kutoka na kazi nzuri anayoifanya ambayo matunda yake yanaonekana kwa
taifa ikiwa ni pamoja na usimamizi mzuri wa majengo.
“Mimi nimeridhia jengo hili
liitwe Samia lakini nimeambiwa hapo nyuma kuna majengo mengine yanajengwa na jengo
moja lipo kwenye hatua nzuri niwaombe likimalizika liitwe Chibunda maana
amefanya kazi nzuri sana sana, hongera
Prof. Chibunda pamoja na Menejimenti yote ya SUA”, amesema Rais Samia.
Aidha Mhe. Dkt. Samia amekitaka
Chuo Kikuu cha SUA kuendelea kulitunza jengo hilo ili liendelee kuwa na viwango
vyenye ubora wa kimataifa na kuwavutia wanafunzi kutoka nje ya Tanzania.
Akitoa taarifa ya Chuo hicho
Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda amesema Chuo cha SUA ni kati ya Vyuo
vikuu vinavyonufaika na mradi wa Elimu ya Juu
kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) na kuishukuru Serikali kwa kukitengea Chuo Sh.
Bilioni 73.6 kupitia mradi huo.
Amesema kwa sasa Mradi upo kwenye hatua
mbalimbali za utekelezaji ambapo kwa upande wa miundo mbinu mradi huo utasaidia
kujenga majengo 9, majengo mawili katika Kampasi ya Mizengo Pinda iliyopo
Katavi, majengo mengine 2 Kampasi ya Solmon Mahlangu na majengo 5 Kampasi ya
Edward Moringe Sokoine.
Aidha katika kuimarisha mafunzo
ya ujasiriamali Prof. Chibunda amesema Chuo hicho kinaendesha Kituo Atamizi kwa
vijana katika kilimo ili kuwajengea uwezo wanafunzi na wadau wengine katika masuala ya kilimo biashara ambapo kwa
sasa Chuo kina vitalu 91 na vitalu 20 vya kilimo cha nje na tayari wameatamia
na kuhitimisha jumla ya wanafunzi 347 katika mafunzo hayo.
“Chuo chetu pia kimeanzisha
mpango wa kuwawezesha wanafunzi kufungua kampuni za ujasiriamali, kupitia
kampuni hizo wanafunzi huja na bunifu mbalimbali ambazo ukitangaza Chuo kitaifa
na kimataifa, juhudi hizo zimeanza kutoa matunda ambapo kampuni moja ya
wanafunzi watano wa Chuo chetu wanamiliki Kampuni ya Mnyama Digital Limited na
tayari wamejishindia tuzo ya kimataifa ya ubunifu bora wa vijana wenye biashara
zinazochipukia”, amesema Prof. Chibunda.
0 Comments