SUAMEDIA

Wanafunzi wa Vyuo vikuu waaswa kupima ili kujua Afya zao

 

Na: George Alexander

Wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Mzumbe wamehimizwa kuweka kipaumbele katika kujilinda na kupambana na maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI ikiwa ni pamoja na kutambua hali zao za afya kwa kupima.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa mkoa wa Morogoro  Bi. Mariam Bendera wakati akifungua Kongamano lililowakutanisha wanafunzi wa elimu ya juu waliopo mkoani Morogoro, lililoenda sambamba na mdahalo wa kupeana elimu kuhusu njia ya kujikinga na maambukizi ya UKIMWI.

Katika mdahalo huo ulionesha vijana asilimia kubwa wenye umri wa miaka 15 hadi 25 wako katika hatari ya kupata maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kutokana na mazingira yanayowazunguka na taarifa wanazozipata kutokuwa sahihi.

Amesema kuwepo wa mijadala kama hiyo kutasaidia kutengeneza uelewa wa pamoja kwa wanafunzi hususani vijana ili waweze kujilinda pamoja na kuilinda jamii kubwa iliyopo nyuma yao na kuweza kufikia malengo yao.

Kwa upande wake Norah Macha ambaye ni mwanafuzi wa Chuo cha SUA ameshukuru kwa kupata elimu ya UKIMWI iliyotolewa kwa vijana na wanafunzi wa chuo hicho pamoja na vyuo vingine kuwa imewasaidia kujitambua na kujikinga dhidi ya UKIMWI pamoja na magonjwa yaambukizwayo kwa njia ya kujaamiana na kuwa ni muhimu kwenda hospitali na kujua afya zao bila uoga.

Mwakilishi wa Ofisi ya Mshauri wa Wanafunzi SUA Bi. Lidyia Bupilipili amesema Chuo kina sera mbalimbali ambazo zinalinda faragha kwa watumishi na wanafunzi suala linaloongeza usalama kwa kila mmoja kwa ustawi wa Chuo na jamii nzima.

Hivyo amewaomba wanafunzi kutokuogopa kufika na kuongea na wataalam ambao Chuo imewaandaa kwa ajili ya kuwasikiliza na kuwasaidia changamoto zao hukue akiwataka wanafunzi hao kutoficha magonjwa na pia kutokuogopa kwenda kuchunguza afya zao .

Kwa upande wake Cyprian Komba ambaye ni mwakilishi wa shirika la NACOPHA pamoja na Shirika la Vijana wanaoishi na VVU amesema kwa takwimu za maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kwa tafiti zilizofanywa na Serikali mwaka 2022/2023 ilikuwa takribani watu 60,000 wamepata maambukizi ya virusi vya UKIMWI kati yao asilimia 40 ni vijana wenye umri wa miaka 15 mpaka 25 na katika asilimia hizo 4o takribani asilimia 80 ya walioambukizwa walikuwa ni mabinti.

Amesema kutokana na takwimu hizo elimu inahitajika zaidi kwa ajili ya kupunguza maambuzi ya virusi hivyo hususani kwa kundi la vijana.

Kongamano hilo lililoandaliwa na serikali ya wanafunzi SUA limefanyika katika chuoni hapo na kuhudhuriwa na wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha SUA na Mzumbe vya mjini Morogoro pamoja na viongozi mbalimbali wa wa SUA na Serikali ambapo shirika lisilokuwa la kiserikali la USAID liliweza kutoa elimu mbalimbali juu ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI.






Post a Comment

0 Comments