Na: Adam Maruma,
Timu ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Mradi wa
Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi - HEET kutoka Chuo Kikuu Cha Sokoine Cha
Kilimo SUA, katika kutekeleza majukumu yake imetembelea msitu wa Mafunzo wa
Ifinga uliopo Halmashauri ya Mji wa Madaba Mkoani Ruvuma pamoja Kampasi ya
Mizengo Pinda iliyopo Mkoani Katavi.
Timu hiyo ikiongozwa na mkuu wa eneo hilo
la mradi Dkt. Emmanuel Malisa na wajumbe wake Jumanne Habibu na Tryphone Ngoja,
ilianza kazi kwa kutembelea katika msitu
wa Ifinga wenye hekta elfu 10 ambapo timu ilifika katika maeneo yaliyopandwa
miti ambayo ni jumla ya hekta 1200, kitalu cha miche chenye miche 155,000
pamoja na eneo linalojengwa mnara utakaotumika kugundua uwepo wa moto katika
shamba.
Dkt. Malisa amesema kazi ya eneo hilo la
mradi ni kufuatilia, na kutathmini maendeleo ya mradi kuelekea kwenye ufikiwaji
wa lengo kuu, na hivyo, wanakusanya taarifa mbalimbali, kuzichakata, na kuandika
taarifa itakayopitishwa kwenye vikao mbali mbali vya Chuo, na baadae
kuwasilishwa Wizarani (Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia).
Mkuu huyo wa eneo la mradi la ufuatiliaji
na tathmini amesema timu imejifunza mambo mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuona
namna Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo - SUA, kinavyoendesha msitu huo mkubwa
wa mafunzo ulioanzishwa mwaka 2018, ambao hakika ni wa msaada mkubwa kwa
wanafunzi pindi wanapokua katika mafunzo ya vitendo.
Dkt. Malisa ameongeza kuwa msitu huo
umekuwepo kabla ya ujio wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi -
HEET, ukiwa chini ya Ndaki ya Misitu, Wanyamapori na Utalii lakini ujio wa
mradi wa HEET umeongeza nguvu ya
uendelezwaji wa msitu ambapo kwa msimu wa mwaka 2023/24 mchango wa mradi wa
HEET umeanza kuonekana kwa ongezeko la ukubwa wa shamba lililopandwa miti toka
hekta 278 msimu uliotangulia (2022/2023) hadi hekta 312, ambalo ni ongezeko la hekta 34, ambayo ni
sawa na asilimia 12.
Ameongeza kuwa katika kitalu cha kuaandaa
miche kuna miti 155,000 (laki
moja na hamsini na tano elfu) ambayo ingepandwa shambani ingetosha kupanda eneo
lenye ukubwa wa hekta 140, na hivyo hekta hizi zikiongezwa kwenye zile hekta 34
zilizopandwa mwanzo, itafanya ongezeko hilo kuwa asilimia 63 ambayo ni mchango
wa Mradi wa HEET katika msitu huo.
Dkt. Malisa amesema lengo la mwanzo
lilikuwa ni kupanda hekta 500 lakini mpaka sasa hekta zilizopandwa ni 312 na
hivyo kasi ya upandaji inatakiwa kuongezwa na kwamba timu yake itajaribu
kuainisha changamoto na namna ya kuweka sawa ili zoezi liendelee vizuri. “…na
hili ndilo lengo kuu la ufuatiliaji; ni kutoa ‘early warning’ ili mradi uweze
kubakia kwenye mstari sawasawa na mpango wake ulioainishwa kwenye andiko la
mradi”.Amesema Dk. Malisa.
Amezitaja baadhi ya sababu zinazopelekea upandaji
wa miti kuwa chini kiwango cha hekta 500
ambazo zilikuwa ndio lengo upandaji wa shamba hilo kwa mwaka kuwa ni changamoto
ya usafiri ambao ungetumika kubeba vibarua kutoka katika makazi yao hadi
shambani, usafiri wa kubeba miche toka kitaluni hadi shambani, na usafiri wa
wasimamizi wa msitu. Hayo yamepelekea kusia mbegu katika kitalu mwezi Oktoba
badala Julai ambao ndio muda unaoshauriwa kitaalam, hali ambayo imepelekea
kushindwa kufikia lengo ka hekta 500.
Katika hatua nyingine, timu hiyo ya Ufuatiliaji
na Tathmini ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi - HEET imetembelea
Kampasi ya Mizengo Pinda ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo iliyopo mkoani
Katavi.
Timu hiyo imekutana na wafanyakazi na
baadhi ya wanafunzi wa kampasi hiyo kwa lengo la kutaka kujua uelewa na
ushiriki wao katika mradi wa HEET, na kujadili changamoto na tahadhari zilizopo
kuhusu mradi.
Dkt. Malisa amesema, uelewa wa wafanyakazi
kuhusu mradi wa HEET ni mkubwa hususan kwenye masuala ya jinsia na wafanyakazi
wameonekana kuridhishwa na ushirikishwaji wao katika mradi. Akizungumza katika
kikao hicho, Naibu Rasi (Mipango, Utawala na Fedha) Profesa Jeremiah Makindara
amesema katika Kampasi hiyo tayari limeanzishwa Dawati la Jinsia na kuna Kamati
ya Uratibu wa Mradi wa HEET.
Kwa upande wake, Bw. Gabriel Mruma ambae ni
mfanyakazi wa Chuo katika Idara ya Miliki, amesema yeye alikua mmojawapo wa
walioshiriki kikamilifu katika zoezi la kufanya tathmini ya athari za
kimazingira na kijamii za mradi, pamoja na zoezi la kutambua maeneo ambako
majengo mbalimbali yatajengwa chini ya Mradi wa HEET. Kupitia kikao hicho, timu
ilipokea pia taarifa kuhusu matarajio ya jamii inayozunguka Chuo kuhusu mradi
ikiwemo kupatikana kwa ajira na kipato kwa makundi mbalimbali kama mama lishe,
vibarua na wamiliki wa nyumba za kupanga.
Kwa upande wa wanafunzi, Dkt. Malisa
amesema kuwa bado kuna changamoto ya uelewa kuhusu mradi huo. Hata hivyo,
wajumbe wa Timu hiyo, Bw. Habibu Jumanne na Tryphone Ngoja walitumia fursa hiyo
kuwapa maelezo kuhusu mradi na namna mradi utakavyoboresha baadhi ya
miundombinu katika Kampasi hiyo.
Katika kuhitimisha vikao hivyo viwili,
wajumbe wa Timu ya Ufuatiliaji na Tathmini walishauri uwepo wa utaratibu maalum
wa kupashana Habari kuhusu Mradi wa HEET katika Kampasi hiyo kwa namna ambayo
hata wafanyakazi au wanafunzi ambao hawakushiriki vikao mbalimbali wataweza
kupata taarifa kuhusu yaliyojiri. Aidha, wanafunzi wameshauriwa kuwa
wanatembelea tovuti ya Chuo ili kujipatia taarifa mbalimbali za Chuo ikiwa ni
pamoja na za Mradi wa HEET.
0 Comments