Na: Farida Mkongwe
Tarehe 23 Julai, 2024 kuanzia saa
2 asubuhi hadi saa 1 jioni, Viongozi, Mfadhili Mkuu na Wadau wa Mradi wa
Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi na Ustahimilivu katika Nyanda Kavu za Kitropiki (Climate Adaptation and
Resilience in Tropical DrYlands-CLARITY) wamekutana jijini Dodoma katika kongamano
la kwanza kwa lengo la kujadiliana juu ya mwenendo wa utafiti unaoendelea
katika mradi huo.
Ili
kufanikisha majadilianao ya utafiti huo timu ya Mradi imetembelea eneo la mradi
lililopo Hombolo pamoja na kukutana na wakulima na wananchi wa eneo hilo ili
kuzungumza nao kwa madhumuni ya kubaini changamoto wanazokabiliana nazo katika
suala la upatikanaji wa maji, kuona shughuli za upikaji wa chumvi katika Kata ya Nzuguni Mtaa wa Mahomanyika. Timu imefika
pia kwenye visima vya Makutupora ambavyo vinatumika kwa kiasi kikubwa kusambaza
maji kwa wananchi wa jiji la Dodoma.
Akizungumza
katika ziara hiyo Kiongozi Mkuu wa Mradi kwa upande wa Tanzania Prof. Japhet
Kashaigili ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti ,
Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalam kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine
cha Kilimo (SUA), amesema wamefanya ziara katika bwawa la Hombolo ambalo
linapokea maji kutoka Makutupora kwa lengo la kuangalia shughuli zinazofanyika
katika bwawa hilo.
“Lakini
pia tumefika hapa kuweza kujifunza kupitia kwa wakulima pamoja na wananchi kwa
ujumla, vile vile kuangalia tathmini za njia za maji na miundombinu yake, kwa
hiyo imekuwa ni fursa nzuri ya watu kuona tunachokifanya kina faida gani kwa
maana ya jamii inayohusika, tumeweza kuona changamoto zilizopo ambazo
zinahitaji suluhisho la kitafiti na tumeyaona mashamba jinsi yanavyolimwa,
tumeona miundombinu inayotumika na hali yake, tumejadiliana na tutaendelea
kujadiliana juu ya kile tulichokiona”, amesema Prof. Kashaigili.
Akizungumzia
eneo la Bonde la Makutupora ambalo ndilo chanzo kikubwa cha maji katika jiji la
Dodoma, Prof. Kashaigili amesema eneo hilo ni muhimu sana na kwamba mradi una
visima ambavyo vinafanyiwa ufuatiliaji, hivyo wametembelea ili kubaini mahusiano
yaliyopo kati ya mwenendo wa maji, jiolojia pamoja na jinsi kuhusianisha na
mito ya maji.
Mtafiti
kutoka SUA Dkt. Joseph Kangile amesema sababu ya kutembelea mtaa wa Mahomanyika Kata ya Nzuguni ambako kina mama wanajishughulisha
na upikaji wa chumvi, ni kwa lengo la
kujionea jinsi jamii hiyo inavyojishughulisha na upikaji wa chumvi ili
kurahisisha kupanga mipango vizuri wakati wa ujenzi wa mabwawa ili maji
yatakayopatikana yasiweze kuwa na chumvi nyingi itakayozuia maji hayo kushindwa
kutumika vizuri kwa matumizi ya nyumbani.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mahomanyika Bw. Ernest Kutona
amesema amefurahishwa sana na watafiti kutoka mradi wa CLARITY kufika katika
eneo hilo na kujionea shughuli za upikaji chumvi ambazo zinafanywa na kina mama
kwa muda mrefu sasa kuanzia miaka 40 iliyopita na kuiomba Serikali iwaboreshee
mazingira kina mama hao kwani kazi hiyo imekuwa ikiwaongezea kipato na kuwawezesha
kuendesha maisha yao.
Bi. Vise
Ndiamo ni mmoja kati ya kina mama wanaojishughulisha na kupika chumvi ambapo
amesema imemsaidia kwa kiasi kikubwa kupata mahitaji yake ukizingatia kuwa yeye
ni mjane na kazi hiyo imemuwezesha kusomesha na kuhudumia familia yake.
Timu
ya CLARITY ikiwa katika eneo la Kata ya Hombolo Bwawani ilipata fursa ya
kumsikiliza Diwani wa Kata hiyo Assed Mathayo ambaye amesema bwawa la Hombolo lina
upana wa Kilomita tatu (03), urefu wa Kilomita kumi na saba (17) na kina cha
mita nane (08). Bwawa hilo linatumika kumwagilia, kunyweshea mifugo na matumizi
mengine lakini hakusita kueleza furaha aliyonayo ya kufikiwa na Timu ya CLARITY
kwani anaamini kuwa watajifunza na yeye pia atajifunza mengi kwa ajili ya maendeleo
ya kata na uendelezaji wa bwawa hilo
Katika kuhakikisha wadau wote
wanashiriki kikamilifu katika utafiti huo, timu hiyo ya CLARITY pia ilikutana
na wakulima wa Zabibu katika kijiji cha Hombolo Bwawani B akiwemo Mary Uguzi na
Ayoub Masima ambao pamoja na kuushukuru
mradi huo kwa nia nzuri ya kuwaendeleza wakulima katika suala la upatikanaji wa
maji, pia wameomba kuendelezwa kwa bwawa
lililopo kwa kulifukua na kutoa udongo uliopo katika bwawa hilo ambao
unasababisha kushindwa kupata maji ya kutosha kumwagilia mashamba yao.
Akizungumzia kuhusu Mradi wa
CLARITY na faida zake, Mhandisi huyo amesema mradi huo ni shirikishi kwa maana
unatoa nafasi ya kujadiliana kwa pamoja changamoto zilizopo na jinsi ya
kuzikabili, hivyo mradi huo utawaongezea kiwango cha uzalishaji wa maji na
kuweza kutunza mazingira na kuyafanya kuwa endelevu kwa vizazi vijavyo.
0 Comments