Na: Edson Kanisa - Katavi
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Halmashauri
ya Wilaya ya Mpimbwe mkoani Katavi zimekubaliana kushirikiana kupitia vyombo
vyake vya habari vya SUA Media na Mpimbwe FM katika kutoa elimu, teknolojia,
ubunifu na matokeo ya utafiti katika sekta ya kilimo.
Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe Bi. Shamim Mwariko akizungumza na ujumbe kutoka SUA (hauko pichani) |
Akizungumza na ujumbe wa SUA uliofika ofisini kwake
Julai 16, 2024 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe Bi. Shamim
Mwariko amesema wamefurahishwa na wazo hilo la SUA kwani ili kuleta maendeleo
ya kilimo nchini ni muhimu wakajua mbinu bora za kilimo.
Amesema kupitia ushirikiano wa SUA na Halmashauri
hiyo utasaidia kufikisha elimu, teknolojia, ubunifu na matokeo ya utafiti huku
akisisitiza watafiti nchini wakiwemo wa SUA kutoa matokeo ya utafiti kwa lugha
rahisi ambayo inaeleweka na mkulima.
Akizungumza wakati akitoa ombi la SUA kushirikiana na Halmashauri hiyo Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko SUA Bi. Suzana Magobeko amesema Menejimenti ya SUA kupitia vikao vyake iliona ni muhimu kuunga mkono juhudi zilizofanywa na Halmashauri hiyo za kuwa na chombo cha habari Mpimbwe FM kwa kutoa maudhui yanayoweza kuwasaidia wakulima na wafugaji ili kuinua sekta hiyo nchini.
Muonekano wa studio za kisasa za Mpimbwe FM |
Bi. Magobeko amesema SUA itahakikisha wataalam wake
katika sekta ya kilimo wanashiriki kikamilifu katika kutoa habari na maudhui kupitia
Mpimbwe FM na SUA Media pia itakuwa ikipokea na kutoa habari za Halmashauri
hiyo kupitia vyombo vyake vya SUA FM na mitandao yake ya kijamii.
0 Comments