SUAMEDIA

Mkutano wa kimataifa wa CLARITY wafanyika jijini Dodoma kutathimini namna ya kutekeleza Mradi kwa mafanikio makubwa

 Na:  Farida Mkongwe

Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi na Ustahimilivu katika Nyanda Kavu za Kitropiki yaani CLimate Adaptation and Resilience in Tropical DrYlands (CLARIT) ni Mradi unaolenga kuongeza usawa, uendelevu na ustahimilivu wa njia za maji za tabianchi katika maeneo kavu ya kitropiki na kuyaingiza masuluhisho yatakayopatikana katika michakato ya kisera na utekelezaji wa kijumuiya.

                        

Hapa nchini, Mradi huo ambao ni wa miaka mitatu na miezi sita ulianza rasmi tarehe 4 Mei, 2023 na kuzinduliwa Oktoba 31, 2023, katika Jiji la Dodoma, jiji ambalo limeendelea kukua, kutanuka na kustawi huku idadi ya watu ikiendelea kuongezeka hali ya kuwa changamoto ya upatikanaji wa maji ambayo ni ya muda mrefu ikiendelea kulikabili jiji hilo.

Mradi wa CLARITY ambao unafanya utafiti jijini Dodoma kwa lengo la kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji unafadhiliwa na Kituo cha Utafiti wa Maendeleo ya Kimataifa (IDRC Canada), Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo (FCDO, Uingereza)  chini ya Mpango wa Kukabiliana na Hali ya Hewa na Ustahimilivu (CLARE)

                    

Katika kuhakikisha malengo ya mradi yanafikiwa, watafiti wote wa CLARITY na Mfadhili Mkuu wanakutana katika kongamano la wiki moja jijini Dodoma kuanzia Julai 22, 2024 kwa lengo la kujadili, kupeana uzoefu na kutathimini namna ya kuutekeleza mradi huo kwa mafanikio makubwa.

                    

Kiongozi Mkuu upande wa ufadhili kutoka Kituo cha Utafiti wa Maendeleo ya Kimataifa (IDRC Canada) Dkt. Bruce Currie-Alder amesema mradi wa CLARITY  ni wa utafiti wa kisayansi ambao umelenga kushirikiana na jamii ili kuwa na masuluhisho ya pamoja ya mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. 

                     

Akitoa salaam katika mkutano uliofanyika Julai 25, 2024 Dkt. Bruce amesema wametoa ufadhili kwa mradi wa CLARITY kwa sababu wanaamini utasaidia kutatua changamoto za kijamii ambapo utafiti utakapokamilika watunga sera nchini Tanzania watatumia matokeo ya utafiti huo katika kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji jijini Dodoma.

Akifungua Mkutano huo kwa niaba ya  Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mkurugenzi wa Rasilimaji za Maji kutoka Wizara hiyo Dkt. George Lugomela amesema pamoja na nchi kuwa na hali nzuri ya upatikanaji wa rasilimali za maji zipatazo mita za ujazo bilioni 126 kwa mwaka, bado mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa vyanzo vya maji unaosababishwa na shughuli za kiuchumi na kijamii na ongezeko kubwa la watu nchini kunatishia kupunguza kiwango cha maji kwa mtu kutoka mita za ujazo 2105 zilizopo na kufikia mita za ujazo 883 ifikapo Mwaka 2035 endapo hatua stahiki hazitachukuliwa.

                                   

Dkt. Lugomela amesema hali hiyo inaweza kuwa mbaya zaidi kwa Nyanda Kavu za Kitropiki ukiwepo mji wa Dodoma kama hakutakuwa na mikakati madhubuti kwani mahitaji ya maji kwa jiji la Dodoma yamefikia lita milioni 149.5 kwa siku wakati uzalishaji ukiwa bado ni lita milioni 79.1 kwa siku.

 “Mradi wa CLARITY umekuja wakati sahihi kwani mchakato unaoendeshwa na wadau wa mradi huo kupitia Maabara za Mabadiliko (Transformation labs) unatoa fursa muhimu nchini kufanya kazi kwa pamoja na kuchukua jukumu la kutafuta suluhisho la upatikanaji wa maji wenye nguvu zaidi, endelevu na usawa katika jiji la Dodoma”, amesema Dkt. Lugomela .

 Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam, Prof. Maulid Mwatawala akitoa salaam kwa niaba ya Makamu wa Mkuu wa Chuo cha SUA Prof. Raphael Chibunda amesema Chuo cha SUA kimekuwa kikishirikiana na wadau mbalimbali katika kutatua changamoto za upatikanaji wa maji zinazoukabili mji wa Dodoma.

                        

“Katika mradi wa CLARITY, SUA inashirikiana na Wizara ya Maji kupitia Kituo cha Umahiri katika masuala ya maji (Water Resources Centre of Excellence) na wadau wengine wa ndani na nje ya nchi katika kuongeza njia za upatikanaji wa maji kwa usawa, uendelevu na ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi katika mkoa wetu wa Dodoma na kuziingiza njia hizi katika michakato ya kisera na utekelezaji na tunaamini suluhisho litapatikana kwa sababu wadau waliopo kwenye mradi huu ni wabobezi katika masuala ya utafiti”, amesema Prof. Mwatawala.

Mwenyeji wa Mkutano huo ni Kiongozi Mkuu wa Mradi kwa upande wa Tanzania Prof. Japhet Kashaigili ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti , Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalam kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), amesema malengo ya kukutana kwao ni kushirikiana, kujadiliana na kupeana taarifa mbalimbali na kuweza kutambua kwa pamoja namna ya kupata majibu wanayoyatarajia kupitia mradi wa CLARITY.

                                      

“Tukiwa kwenye jukwaa hili la mabadiliko tunajaribu kuangalia njia tutakazotumia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji kwa jiji la Dodoma, kusikia na kupata mawazo ya wadau ambayo mradi utatumia katika kufikia utatuzi na kuainisha maeneo ya ushirikiano kwa sababu CLARIY inajumuisha na nchi nyingine nje ya Tanzania”, amesema Prof. Kashaigili.

Naye Kiongozi wa Masuala ya Tabianchi nchini Tanzania kutoka Shirika la Maendeleo la Uingereza (FCDO, UK) Dkt. Catherine Pye amesema Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania unafanya kazi vizuri na Mradi wa CLARITY na umejionea athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi ambayo yamesababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi pamoja na kuathiri pato la Tanzania.

                                                                                                                                

Amesema kupitia mkutano huo watapata fursa ya kujadili kuhusu mabadiliko ya tabianchi , kubadilishana utaalamu na kufanya tafiti zitakazotatua changamoto hizo ambazo nyingine zimesababishwa na shughuli za kibinadamu zikiwemo kilimo kwenye vyanzo vya maji na ukataji wa miti kiholela kwa ajili ya matumizi ya mkaa.

Prof. Richard Taylor Kiongozi wa mradi wa CLARITY kutoka nchini Uingereza amesema wanakutana na changamoto ya kuboresha mazingira kwa sababu mazingira hayo yamekuwa na ukame kwa muda mrefu lakini kwa sababu CLARITY inashirikisha wadau wa nchi mbalimbali kutoka nchi za  Tanzania, India, Niger na Nigeria watahakikisha wanatumia ubunifu katika kugundua tatizo na kuihusisha jamii ili kutumia mifumo itakayosaidia kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

                                      

Prof. Taylor amesema kupitia Maabara ya Mabadiliko ( Transformation labs), watafiti watapeana maarifa na kufanya tathmini ya upatikanaji wa maji katika maeneo ya nyanda kavu za kitropiki na anaamini kuwa watafanikiwa kutatua changamoto hiyo.  


Akifunga mkutano huo kwa niaba ya Katibu Tawala mkoa wa Dodoma Bw. Kaspar Mmuya, Katibu Tawala Msaidizi Bi. Aziza Mumba amekishukuru Chuo cha SUA pamoja na wadau wote wa CLARITY kutoka ndani na nje ya Tanzania na kusema kuwa anaamini matokeo ya utafiti wa mradi huo yatatatua tatizo la upatikanaji wa maji, utunzaji wa vyanzo vya maji na changamoto zingine zinazopelekea kuwa na upungufu wa maji katika mji wa Dodoma.


     

 

 

 PICHA NA TATYANA CELESTINE

ZAIDI BOFYA LINK HAPO CHINI

 https://tatyana35.pixieset.com/clarityconsortiumdodomat-labmeeting-program/day3/

 

Post a Comment

0 Comments