SUAMEDIA

Tutalipa fidia ili watu wapishe maeneo kwa ajili ya SUA - Rais Samia Suluhu Hassan

 Na: Gerald Lwomile

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuwa Serikali yake italipa fidia ya Shs. Bilioni 1 na Milioni 700 kwa wananchi ili wapishe katika eneo kwa ajili ya upanuzi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Kampasi ya Mizengo Pinda mkoani Katavi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia maelfu ya wananchi wilayani Mpimbwe

Rais Samia ametoa ahadi Julai 15, 2024 katika ziara yake ya kikazi katika kata ya Kibaoni wilayani Mpimbwe wakati akijibu hoja ya Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Pinda aliyemuomba Mhe. Rais kusaidia kulipwa kwa fidia hiyo kwa wananchi.

Katika hoja yake Mhe. Pinda amesema eneo hilo lenye ukubwa wa Hekta 240 au Ekali 580 limekwama kuendelezwa na SUA kutokana na kukosa fedha pamoja na kuwepo kwa juhudi zinazofanywa na Menejimenti ya SUA chini ya Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda.


"Katika kuhangaika hangaika nikakutana na Prof. Chibunda tena kwa bahati nzuri Mhe. Rais, Prof. Chibunda mwenyewe yuko hapa, nikamuomba aje na timu yake waangalie kama eneo hili linafaa kuwa Chuo, akaja na wakakubali na kusema wanakuja mara moja……, amekuwa akihangaika sana kupata fedha huku na huku ili kuongeza ukubwa wa eneo kwa kuwafidia wananchi ili litumie kujenga mabweni na madarasa mengine kwa ajili ya wanafunzi"

Amesema Kampasi hiyo iliyopo chini SUA imekuwa mkombozi kwa wananchi wa Mkoa huu kwani sasa watoto watawatapa elimu hasa katika uzalishaji wa mazao, ufugaji wa nyuki na mazao yake lakini uhifadhi wa wanyama kutokana na kuwepo kwa Hifadhi ya Katavi ambayo ina wanyama wakubwa kuliko maeneo mengine.

Baadhi ya mamia ya wakazi wa wilaya ya Mpimbwe wakimsikiliza Rais Samia

Akijibu hoja nyingine ya Pinda kuhusu Hifadhi ya Katavi Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameseme yeye mwenyewe atakuja kufanya Royal Tour sehemu ya pili katika Hifadhi hiyo ambayo ameona ina wanyama wengi na wakubwa wanaovutia sana ili kufungua utalii katika eneo ukanda huu.

Rais Samia amemaliza ziara yake ya siku nne katika mkoa wa Katavi ambapo amewapongeza viongozi na wananchi mkoani humo kwa kudumisha amani na kuwataka wahamiaji katika eneo kuhakikisha wanaendeleza amani waliyoikuta

Picha chini ni viongozi wa SUA wakisalimiana na Mawaziri mbalimbali waliokuwa katika ziara ya Mhe. Rais 👇





Picha chini ni baadhi ya wafanyakazi wa Kampasi ya Mizengo Pinda walioshiriki katika mkutano wa Mhe. Rais 👇




Post a Comment

0 Comments