SUAMEDIA

Wataalamu wa tiba za wanyama wametakiwa kutumia elimu waliyonayo kutatua changamoto za afya ya mifugo

 

Na: Ayoub Mwigune

 

Wataalamu wa tiba za wanyama nchini wametakiwa kutumia mafunzo na elimu wanayopata kuhusu tiba za wanyama ili kuongeza ufanisi kwenye utendaji kazi ikiwa ni pamoja na kufuatilia magonjwa yatokayo kwa Wanyama kwenda kwa Binadamu sanjari na kutatua changamoto za afya ya mifugo.



Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia mambo ya Afya ya Jamii katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutoka Idara ya Huduma ya Mifugo Dkt. Stanford Balema wakati akifunga mafunzo ya watalaamu wa tiba ya wanyama yaliyofanyika kwa takribani mwezi mmoja mjini Morogoro.

Dkt. Stanford amesema kupitia mafunzo hayo wanategemea washiriki wakiwemo waatalamu wa mifugo wataweza kutekeleza majukumu yao sambamba na kupata taarifa za magonjwa ambapo kupitia taarifa hizo Wizara itaweza kupata njia ya kutafuta utatuzi na udhibiti wa changamoto kwa mifugo.

 Katika hatua nyingine Dkt. Stanford amewaomba washiriki hao kukitumia Chuo cha SUA katika kujiendeleza kitaaluma ili kuwa wabobezi bora zaidi katika Magonjwa ya mifugo huku akiishukuru SUA na FAO kwa kutoa ushirikiano wao thabiti kwa Serikali kwa kuendelea kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya ya wanyama na binadamu nchini.

Dkt. Moses Ole-Nesele ambaye ni Mratibu wa mafunzo ya ufuatiliaji wa magonjwa ya wanyama yaani (In Service Applied Veterinary Epidemiology Training–ISAVET) upande wa FAO ameeleza kuwa madhumuni ya mafunzo hayo kwa watumishi wa umma ni kuweza kufuatilia magonjwa yatokanayo na wanyama lakini pia kuripoti magonjwa kwa wakati, na kutoa taarifa ambazo zinaweza kulinda mifugo na jamii kwa ujumla. 

‘’Tunapotaka kufanya biashara ya nyama na maziwa ni lazima tuhakikishe mifugo yetu ipo salama kwenye afya zao ili kuongeza wanunuzi wengi, tusipo fanya hivi hakuna mtu yeyote atakaye ingia nchini kwetu na kufanya manunuzi ya bidhaa isiyo na ubora, magonjwa ya mlipuko yamekuwa yakijirudia rudia mara kwa mara na mengine kuingia mapya. hivyo mafunzo haya yatapunguza magonjwa na kutoa elimu kwa umma ili kutokomeza milipuko ya magonjwa na ufugaji holela’’ , amesema Dkt. Moses Ole-Nesele

Kwa upande wake Khamisi Haji Mbwembwe Daktari Msaidizi kutoka Wilaya ya Kaskazini A Unguja, amesema mafunzo hayo yatamsaidia yeye pamoja na watumishi wengine kufuga mifugo bora yenye afya na wananchi kupata nyama na maziwa yaliyokuwa katika ubora wa hali ya juu.







Post a Comment

0 Comments