SUAMEDIA

SUA yapongezwa kuitunza Kampasi ya Solomon Mahlangu

 Winfrida Nicolaus

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimepongezwa kwa kuifanya Kampasi ya Solomon Mahlangu kuwa kituo cha mafunzo ambacho kinawasaidia vijana wa Kitanzania kufikia malengo yao kitaaluma huku miundombinu ikiendelea kuhifadhiwa kwa ajili ya historia na alama ya uhusiano wa kindugu, kirafiki na ushirikiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini.

Spencer Hodgson (kulia) na ujumbe wake alipotembelea Kampasi ya Solomon Mahlangu (kushoto) ni  Dkt. Geoffrey Karugila Rasi wa Ndaki ya Solomon Mahlangu (Picha zote na Ayoub Mwigune)

Amebainisha hayo Bw. Spencer Hodgson mmoja wa wasanifu wa majengo na miundombinu wakati harakati za ukombozi wa Afrika ya Kusini alipotembelea katika Kampasi ya Solomon Mahlangu mjini Morogoro Juni 10, 2024 ambapo amesema sehemu hiyo ni ya muhimu kwa maisha yao kwa kuwa waliishi katika eneo hilo.

Anasema amefurahi kuona eneo hilo lililokuwa pori sasa ni sehemu ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, akisema wakati wanaondoka maeneo mengi yalikuwa wazi kwa lengo la kuwasaidia kuona adui na kukimbia ambapo sasa eneo hilo limeboreshwa na kuendelezwa katika historia.

“Nimefurahi kuja Tanzania zaidi katika eneo ambalo lilikuwa sehemu ya maisha yangu, nimetembea na kuona jinsi eneo lilivyoboreshwa zaidi kwa kujengea majengo mapya, kupanda miti na kuitunza vizuri sehemu hiyo ya kihistoria inapendeza sana hapa ndipo mahali tulipoanzia na baadaye kwenda Dakawa hivyo nasikia fahari kuwa mahali hapa”, alisema Hodgson ambaye alikuwa sehemu ya wasanifu majengo yaliyopo eneo la Solomon Mahlangu.


Naye mwenyeji wake Dkt. Geoffrey Karugila kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda amesema kuwa ujio wa wageni mbalimbali kutoka Afrika ya Kusini unaonesha dhahiri  mahusiano mazuri baina ya nchi hizo mbili akisema mahusiano hayo yanafanya SUA kuwa sehemu ya kihistoria ambayo inaendelea kuenea siku hadi siku na kukitangaza Chuo.

“Spencer Hodgson alikuja miaka ya 79 akiwa na familia yake huku binti yake akiwa na umri wa miaka tisa (9) tu hivyo alisoma hapa kwa kuwa waliishi hapa hapo utaona ni namna gani ujio wao umeweza kutusaidia kujua mambo mengi zaidi na ya faida ya kutuwezesha kuendelea kuitunza sehemu hii ya kihistoria si hivyo tu wageni wanapoendelea kuja chuoni kwetu tunajitangaza pia kwa kuwa sisi ni sehemu ya historia hivo kwa kuwa tupo kwenye eneo hilo”, alisema Dkt. Karugila.

Ugeni huo mbali na kutembelea majengo mbalimbali waliyokuwa wanatatumia kipindi hicho cha kupigania uhuru kama Ukumbi wa Nelson Mandela Freedom Square pia wametembelea makaburi ya Wapigania Uhuru wa Chama cha ANC.





Post a Comment

0 Comments