Na: Asifiwe Mbembela
Washiriki wa semina ya kitaalamu ya uzalishaji wa mvinyo nchini wameaswa kuwekeza muda wao katika kujifunza namna nzuri ya kuandaa na kuzalisha divai bora ili iweze kushindana na bidhaa kama hizo ambazo zinazalishwa na mataifa shindani.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Shahada za Uzamili, Utafiti Uhauwilishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Japhet Kashaigili wakati akifungua mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa ushirikiano na TARI-MAKUTOPORA, Kiwanda cha Utengenezaji wa Mvinyo cha Alkovintage na Ushirika wa Wakulima wa Zabibu na Masoko (UWAZAMAM) yaliyofanyika Jijini Dodoma.
Prof.
Kashaigili amesema uzalishaji wa mvinyo una mahitaji makubwa kwa watumiaji wa
ndani na nje ya nchi hivyo kama kutakuwa na uzalishaji wenye kuzingatia viwango
vizuri, mvinyo wa Tanzania utaweza kuwa soko hata nje ya mipaka ya nchi tofauti
na hali ilivyo kwa sasa.
“Ukipita
kwenye maeneo mengi hapa Dodoma, huwa naona chupa mbalimbali za mvinyo, lakini
nyingine zina nembo ya nje sasa unajiuliza tutaweza kushindana nao kwa ubora na
bei, sasa kama wazalishaji wa ndani ni lazima tuambiane ukweli kuwa tujikite kwenye
kuzalisha mvinyo wenye ubora ambao utauzika hata nje ya nchi bila shida”,
alisema Prof. Kashaigili.
Ameongeza
kuwa uzalishaji wa mvinyo kwa miaka ya sasa ni chanzo kikubwa cha mapato hivyo
uwekezaji mzuri katika uzalishaji utaongeza kipato pamoja na kuongeza mtandao
wa fursa (networking) baina ya wazalishaji na wataalamu.
Mtafiti
Mwandamizi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI - MAKUTUPORA) Felista
Joseph Mpore akiongea katika semina hiyo pamoja na kuhimiza umuhimu wa kuchagua
zabibu bora wakati wa uandaaji pia ameeleza namna sukari ilivyo na athari
chanya ama hasi katika kuufanya mvinyo kuwa mzuri.
Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI - MAKUTUPORA) Felista Mpore akitoa mafunzo katika semina hiyo |
Kwa upande wake, Prof. Bendantunguka Tiisekwa Mwezeshaji katika semina hiyo akiwa ni Mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo ya Biashara na Usindikaji wa Chakula, ameeleza kuwa ili miradi ya wazalishaji wa divai iweze kudumu na kuwa na tija ni umuhimu shughuli zao zizingatie matakwa na sheria na kanuni zilizopo, ikiwemo usalama wa mlaji.
Prof. Bendantunguka Tiisekwa akiwasilisha mada katika semina hiyo kuhusu masuala ya sheria
Mafunzo kwa wazalishaji wa mvinyo yanafanyika chini ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) ukiwa ni mkakati wa Chuo kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuongeza uzalishaji wa mvinyo kupitia viwanda, elimu, ujuzi na maarifa mbalimbali yanayoendelea kutolewa na SUA.
Picha mbalimbali za washiriki wa ya wazalishaji wa mvinyo (picha zote na Asifiwe Mbembela)
0 Comments