Na: Gerald Lwomile
Imeelezwa kuwa Shahada ya Uzamivu ya Sayansi ya Misitu chini ya Mradi wa (REFOREST) inayotolewa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ni ya kipekee na itatoa wahitimu wabobevu katika sekta ya misitu na kusaidia kutunza na kulinda misitu hasa katika nchi zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Haya
yamesemwa Juni 13, 2024 na Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, na
Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Japhet Kashaigili
wakati akifungua warsha ya uwasilishaji wa matokeo ya utafiti kwa wanafunzi wa
Shahada ya Uzamivu kutoka SUA.
Prof.
Kashaigili amesema wanasayansi hao wabobevu katika sekta ya misitu pamoja na
kupata mafunzo lakini pia wamefanya utafiti katika nchi zao na kuwa mbinu hiyo
ililenga kuimarisha ubora na kuongeza idadi ya wanasayansi wenye uwezo wa kufanya
utafiti na kuwezesha wahitimu katika ukanda wa Jangwa la Sahara kuwa na ushirikiano
katika uhifadhi wa misitu.
Prof. Japhet Kashaigili akifungua warsha hiyo |
Amesema
warsha hizi za uwasilishaji wa matokeo ya utafiti hujenga daraja na kuwajengea
uelewa wanasayansi na hata watunga sera wakati wa kushughulikia masuala muhimu, kutoa na kusambaza
maarifa mapya ili kuleta maendeleo kupitia matokeo ya utafiti.
Akizungumzia utafiti wake Bi. Jacquline Kajembe Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu aliyefanya utafiti wa kuangalia mnyororo wa thamani katika viungo amesema ili kuwa na uzalishaji mzuri wa viungo inahitajika misitu endelevu na ndiyo maana maana maeneo ya Amani wilayani Muheza mkoani Tanga na maeneo ya Milima ya Uluguru ambapo ndiko amefanyia utafiti wake yamekuwa na ufanisi mkubwa katika uzalishaji wa viungo na kuwa jitihada zinatakiwa kuoongezwa katika kuwaelimisha wakulima kuhakikisha wanalima kilimo cha kisasa pasipo kuharibu misitu.
Naye
mwanafunzi kutoka Rwanda Bw. Elias Nelly Bapfakurera amesema kuwa miti iliyopo kwenye kilimo mseto ina
umuhimu mkubwa kwenye upatikanaji wa kuni za kupikia pamoja na kukabiliana na
mabadiliko tabia nchi.
Kabla
ya kumkaribisha mgeni rasmi ili kufungua warsha hiyo Mratibu wa Mradi wa
REFOREST Prof. Romanus Ishengoma amesema wanafunzi hao wa Shahada ya Uzamivu
wamefanya utafiti katika nchi zao na wanatarajia matokeo hayo ya utafiti
yatazinufaisha nchi zao na hasa katika nyororo mzima wa thamani wa ukuaji wa
misitu.
Mratibu wa Mradi wa REFOREST Prof. Romanus Ishengoma akizungumza katika warsha hiyo |
0 Comments