SUAMEDIA

Kampuni ya Kiwanda cha Kuzalisha Sukari cha Kilombero yazindua kampeni kubwa ya kushirikisha wakulima kuimarisha maendeleo ya wakulima

 

Na: Calvin Gwabara - Kilombero.

Kampuni ya Kilombero Sugar imezindua kampeni ya Ushirikishaji wakulima na uwekezaji kama sehemu ya Mradi wake wa Kupanua kiwanda cha K4 yenye lengo la kuimarisha maendeleo miongoni mwa wakulima wa miwa kupitia mawasiliano ya kimkakati na ushirikiano na wadau.

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Mhe. Dunstan Kyobya (Kulia) na Mkurugenzi wa Wakulima wa nje Kilombero Sugar Pierre Redinger  wakati wa uzinduzi wa Kampeni hiyo.

Akizundua kampeni hiyo Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Mhe. Dunstan Kyobya, amepongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Kiwanda cha sukari cha Kilimbero kupitia kampeni ya Kuinua Wakulima kwa kuwa inathibitisha tena kujitolea kwake katika kuwekeza kwa watu, mafunzo, teknolojia na kuweka kiwango kipya cha kilimo nchini Tanzania.

 "Mpango huu wa Kupanua kiwanda cha K4 na kampeni ya Kuinua Wakulima ni jambo muhimu kwa kipato endelevu kitakachoboresha maisha ya wakulima wa miwa katika Bonde la Kilombero na  Serikali imejitolea kutengeneza mazingira mazuri kwa uwekezaji wa biashara na ustawi wa jamii" alisema Mhe.  Kyobya.

Amefanua kuwa kutokana na changamoto za msimu uliopita zilizosababishwa na mvua kubwa zilizopelekea El Nino, Kiwanda hicho kimechukua hatua madhubuti ya kuwatuliza na kuwaliwaza wakulima kupitia mradi huo wa upanuzi wa kiwanda cha K4. ambao hadi sasa umefikia 90%, na kwamba huo ni uwekezaji mkubwa kuwahi kufanywa na illovo barani Afrika.

Amesema kuwa mradi huo mkubwa unathibitisha imani ya kampuni kwa jamii ya wakulima wa ndani, ambao watazalisha 60% ya miwa inayohitajika katika kiwanda hicho.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo Mkurugenzi wa Wakulima wa nje Kilombero Sugar Pierre Redinger  alitangaza kuwa Kiwanda cha sukari Kilombero kimejitolea kutoa mkopo wa mbegu za miwa tani 20000 kwa wakulima, kwa msimu wa upandaji wa 2024/25 na 2025/26, ambao utasaidia zaidi upanuzi huo.

 “Uwekezaji wetu katika Mradi wa Kupanua kiwanda cha K4 unatokana na imani tuliyonayo kwa wakulima wetu, safari hii ilianza mwaka 2018 kwa usajili wa wakulima, ukiungwa mkono na Ofisi ya Wilaya ya Kilombero, ambao ulifungua njia kwa biashara hii muhimu."alieleza Redinger.

Kwa upande wake Muwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania, Bw. George Gowelle, ameelezea mchango mkubwa wa serikali katika mradi huu, akisema kuwa serikali itaendelea kuunga mkono juhudi zinazolenga kuongeza utoshelevu wa sukari na kwamba Kilombero Sugar imeweka mfano wa kuigwa, na serikali itaendelea kuunga mkono jitihada kama hizi."

Nae Bakari Iddi Mkangama, Mwenyekiti wa Kilombero Joint Enterprises Cooperatives Society, inayowakilisha AMCOS 17 zinazofanya kazi moja kwa moja na Kilombero Sugar, amepongeza kampeni hiyo na kuona kama fursa ya mabadiliko.

"Mpango huu utaleta mabadiliko makubwa kwa soko letu kuwa la kuaminika, kipato endelevu, na kuboresha maisha hivyo tunapaswa kuchangamkia fursa hii adhimu” alisema Mkangama.

Kampeni hiyo iliyozinduliwa kwenye mashamba ya miwa ya Kilombero na kuhudhuriwa na wadau wengi ikiwemo wasimamizi, Viongozi wa serikali za mitaa, na wakulima wa miwa ambao wote ni viungo muhimu katika mnyororo wa thamani wa kilimo cha miwa nchini imebeba Kauli mbiu isemayo  "Soko la kuaminika, kipato endelevu, na kuboresha maisha”.

Wadau wakipata maelezo wakati wa hafla ya uzinduzi wa kampeni hiyo.



Post a Comment

0 Comments