Na: Tatyana Celestine
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
(SUA) kimeendelea kupongezwa kwa kuzidi kuzalisha wanafunzi walio bora katika
soko la ajira na kuonesha matokeo chanya katika kazi hivyo kufanya Sekta ya
kilimo na viwanda kukua kwa kuzingatia ubora na kuwategemea wanafunzi hao
kupelekea kukiwakilisha vema chuo hicho duniani na kutengeneza taswira kwamba
wanahitajika katika maeneo mbalimbali ndani nje ya nchi.
Hayo yamesemwa katika Kikao cha Kamati
ya Ushauri wa Viwanda kilichojumuisha washiriki kutoka Taasisi na makampuni
mbalimbali nchini pamoja na SUA lengo likiwa ni kupitia shughuli zilizofanywa
na kitengo cha mashirikiano ya viwanda na kutoa ushauri wa mpango kazi katika mwaka ujao ambacho
kimefanikiwa kwa kujipambanua kuona wanawezaje kuwa mabalozi wa mabadiliko pamoja
na kuchochea, kuhamasisha urithi wa
teknolojia mpya kwa kutumia njia mbalimbali kama majadiliano, na vyombo vya habari.
Akizungumza na suamedia mara baada ya kikao hicho Mkurugenzi wa Mawasiliano Makampuni ya Bakhresa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Ushauri wa Viwanda SUA Bw. Hussein Ally amesema kuwa wahitimu kutoka SUA wamekuwa wakifanya vizuri katika maeneo mbalimbali hii inaonesha wamepata mafunzo vizuri kwa kukabiliana na soko la ajira hivyo makampuni na maeneo mengine ya kazi nchini wameshauriwa kuwachukua wahitimu hao bila ukakasi wowote kutokana na uelewa, uwajibikaji pamoja na ujuzi wa teknolojia mpya.
Aidha ameongeza kuwa makampuni ya
Bakhresa yataendelea na utaratibu wa kuwapokea wahitimu katika mafunzo kwa
vitendo kwani wao hawana hofu wala sababu ya kuficha teknolojia zao wanaamini
wao kwa kufanya hivyo wanatoa mchango mkubwa katika kukuza vijana kikazi, sekta
ya viwanda na kilimo kupitia utekelezaji wao kwa weledi na ufanisi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni
ya Intermech Engeneering LTD, Mhandisi Petter Chisawillo amesema kuwa wamekuwa na mahusiano na SUA kwa
muda mrefu kupitia bidhaa mbalimbali ikiwemo, mihogo , kusambaza teknolojia za
usindikaji wa mihogo vijijini pamoja na kuwapokea wanafunzi wa SUA kufanya
mafunzo kwa vitendo kwani kwa kufanya hivyo inawasaidia wao kupata maarifa
ambayo wasingeweza kuwanayo kama wangefanya wenyewe.
Mhandisi huyo amesema kuna uhitaji wa wao kuzidisha ushirikiano wa pamoja katika kutatua changamoto
zinazojitokeza hasa katika suala zima la teknolojia rahisi kwa ajili ya kuweka
mitambo ya kusaidia kilimo kuanzia mashambani mpaka usindikaji wa bidhaa, kufanya
ubunifu, utafiti na kuweka maarifa ili viwanda viweze kujua ni kitu gani
kinaweza kusaidia vijijini kwa maana hiyo ni njia sahihi ya kuinua
kilimo nchini.
Alipotakiwa kuzungumzia namna
gani mkulima mdogo anaweza kunufaika kutokana na wao kuwa wajumbe katika kamati ya Ushauri wa Viwanda Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mtandao wa Wakulima Wadogo
Tanzania (MVIWATA) Bw. Stephen Ruvuga amesema lengo la kufanya tafiti na
mipango katika sekta ya kilimo ni kuelekeza kwa mkulima mwenyewe hivyo kila
kinachofanyika kinaakisi ndoto, maendeleo, malengo kwa mkulima sambamba na wao kama chombo wameona kuna ombwe katika
elimu inayotolewa vyuoni na mkulima mwenyewe hivyo kwa wao kutoa ushauri
unaoakisi uhalisia kupitia kamati hiyo inaleta matumaini katika kutatua
changamoto kwenye sekta ya kilimo na viwanda.
Naye Naibu Mratibu wa Mradi wa
Elimu ya Juu kwa Mabadiliko ya Kiuchumi (HEET) SUA Dkt. Winfred Mbungu amesema Taasisi
ya Elimu ya juu inatakiwa kuendana na mabadiliko ya Teknolojia pasi kuachwa
nyuma na Tasnia hivyo kikao hicho kimelenga kusaidia wahitimu wa SUA kuweza
kufaidika kwa namna mahitaji ya viwanda yanaweza kutekelezwa kupitia wahitimu
wao kwani wao wanatakiwa kuzalisha wafanyakazi au waanzilishi wa viwanda na
biashara ndio sababu kupitia mradi huo wamejitahidi kuhimarisha miundombinu ya
ufundishaji kama vile karakana na maabara pamoja na kuboresha mashirikiano yao
na sekta binafsi ili kutumia teknolojia zao.
Aidha kupitia kikao hicho SUA
imeendelea kushauriwa kuzidi kutengeneza mashirikiano na makampuni mengine
ikiwemo Bagamoyo Sugar ili kuongeza wigo katika kusaidia maendeleo ya viwanda
katika kuzalisha wataalamu walio na weledi wa kutosha katika kila eneo
linalohusu kilimo na uwekezaji na kwamba itasadia kujua ni kwa namna gani wanaweza
kutoa elimu hiyo katika ubora pamoja na kubaini teknolojia mpya ambazo
zitarahisisha kukua kwa Uchumi wa nchi na sekta ya kilimo kwa ujumla.
PICHA ZAID BOFYA HAPA
0 Comments