SUAMEDIA

SUA yapongezwa kwa kupeleka Mradi wa CLARITY Dodoma


Na: Farda Mkongwe

Katibu Tawala mkoani Dodoma Bw.  Kaspar Mmuya amekishukuru na kukipongeza Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kuanzisha Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi na Ustahimilivu katika Nyanda Kavu za Kitropiki (CLARITY) ambao unafanya utafiti utakaosaidia kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji jijini Dodoma.

                                                        

Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Katibu Tawala huyo katika Warsha ya Maabara ya Mabadiliko iliyofanyika jijini Dodoma, Katibu Tawala Msaidizi Sekta ya Uchumi mkoani Dodoma Bi. Aziza Mumba amesema kwa sasa chanzo kikubwa cha maji kinachotegemewa jijini Dodoma humo ni visima vilivyo kwenye bonde dogo la Makutupora ambavyo vinaendelela kulindwa ili wananchi wasiendelee kuvivamia.

                                

Amesema utafiti uliofanyika hivi karibuni umebainisha kuwa asilimia 51 ya hifadhi ya maji ya bonde la Makutupora imevamiwa kwa shughuli za kibinadamu na kwamba utafiti huo umewafanya waendelee kuweka mikakati mingine ya kuimarisha ulinzi zaidi wa bonde hilo la Makutupora ambalo kwa sasa linatoa takribani asilimia 90 ya maji yote yanayotumika jijini Dodoma.

                                       

Akizungumzia mipango mbalimbali ya kuhakikisha maji yanapatikana jijini humo Katibu Tawala huyo amesema Serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi wa maji wa Bwawa la Farkwa na kwamba wanatarajia mradi huo ukikamilika utaongeza hali ya upatikanaji wa maji katika jiji hilo.

                                    

Amesema mpango wa muda mrefu ni kuleta maji Dodoma kutoka Ziwa Victoria lililopo Mwanza lakini mpango wa muda wa kati ni utekelezaji wa mradi wa maji wa bwawa la Farkwa na mpango wa muda mfupi ni kuendelea kutafuta vyanzo vingine vya maji katika maeneo mbalimbali. 

Picha na Tatyana Celestine









Post a Comment

0 Comments