Imeelezwa kuwa Maabara ya Mageuzi iliyopo chini ya Mradi wa
Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi na Ustahimilivu katika Nyanda Kavu za
Kitropiki (CLARITY) ambayo inashirikisha
wadau mbalimbali wanaotafuta suluhisho za changamoto ya mabadiliko ya tabianchi
na athari zake katika upatikanaji wa maji ya ardhini inaweza kusaidiakutatua changamoto ya upatikanaji wa maji
jijini Dodoma.
Hayo yameelezwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam,
Prof. Maulid Mwatawala wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Warsha ya Maabara ya Mabadiliko iliyofanyika
jijini Dodoma.
Prof. Mwatawala amesema changamoto ya upatikanaji wa
maji jijini Dodoma ni ya muda mrefu kutokana na jiji hilo kuwa katika eneo
ambalo ni nyanda kavu na ndiyo sababu mradi wa CLARITY uliona umuhimu wa kufanya
utafiti wa kuangalia maji yaliyopo ardhini namna ya kuyatunza, kuyasambaza kwa
upatikanaji ambao utakuwa wa kiusawa kwa jinsia zote na makundi yote na pia uwe
ni endelevu na wa uhakika.
“Kundi hili imekaa hapa kuangalia nini utakuwa mchango
wa maji yaliyopo ardhini katika kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji hapa
Dodoma ikihusisha pia vyanzo vingine, sasa wadau hawa wamekutana ili kutoa
suluhisho la pamoja, jambo mojawapo tunaloliangalia kwa sasa ili tuweza kwenda
mbele ni lazima tutunze vyanzo vya maji vilivyopo na ambalo wanalizungumzia
wadau hapa ni upandaji wa miti na kuitunza kwa sababu miti ikipandwa
isipotunzwa inapotea”, amesema Prof. Mwatawala.
Kwa upande wake Mkuu wa Mradi huo na Mkurugenzi wa Kurugenzi ya
Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu SUA Prof.
Japhet Kashaigili amesema Maabara ya Mageuzi ya
CLARITY mjini Dodoma inaongozwa na SUA huku akibainisha kuwa CLARITY imelenga
kuongeza usawa, uendelevu na ustahimilivu wa njia za maji za tabianchi katika
maeneo kavu ya kitropiki na kuyaingiza masuluhisho yatakayopatikana katika michakato
ya kisera na utekelezaji wa kijumuiya.
Naye
Mtaalamu wa Maji chini ya Ardhi kutoka Bonde la Maji la Wami Ruvu Ezra
Mwakabumbe amesema katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi
wao wamepanda miti 17,600 kwa mwaka huu na kutoa hamasa kwa watu mbalimbali
kuendelea kupanda miti na kuhifadhi vyanzo vya maji.
“Pia
tumeunda jumuiya za watumiaji maji ambazo zimekuwa na msaada mkubwa kwetu
kuweza kutupatia taarifa za watu wanaovamia vyanzo vya maji lakini pia
tumeingia makubaliano na JKT Makutupora kufanya doria mara kwa mara kwenye ile
hifadhi ya maji ili kudhibiti mifugo na shughuli za kibinadamu zisiweze
kufanyika ndani ya hifadhi ya maji”, amesema mtaalamu huyo.
Mradi wa
CLARITY ambao ni wa miaka mitatu na miezi sita ulianza mwaka 2023 na unafadhiliwa na Kituo cha Utafiti wa
Maendeleo ya Kimataifa (IDRC Canada), Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo (FCDO, Uingereza) chini ya mpango wa Kukabiliana na Hali ya
Hewa na Ustahimilivu (CLARE).
0 Comments