SUAMEDIA

Maabara ya Mabadiliko ya Mradi wa CLARITY-SUA yaendelea na utafiti wa kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji Dodoma

 Na: Farida Mkongwe

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi kimeendelea kufanya tafiti ili kupata majawabu ya changamoto mbalimbali za upatikanaji wa maji katika Jiji la Dodoma kwa kutumia Maabara ya Mabadiliko (Dodoma Transformation lab).


Kauli hiyo imetolewa Juni 20, 2024 jijini Dodoma na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam, Prof. Maulid Mwatawala wakati akifungua Warsha ya Maabara ya Mabadiliko chini ya Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi na Ustahimilivu katika Nyanda Kavu za Kitropiki (CLARITY).

                                 

Prof. Mwatawala amesema pamoja na SUA kutoa Astashahada na Shahada mbalimbali za Uzamili na Uzamivu, pia kinafanya tafiti zinazolenga kutatua changamoto mbalimbali nchini ikiwemo changamoto ya upatikanaji wa maji ambapo madhara ya changamoto hii yamekuwa yakijionesha dhahiri katika maeneo mengi ya nchi na kwamba hali inaweza kuwa mbaya zaidi kwenye maeneo ya nyanda kavu na kame za kitropiki kama mkoa wa Dodoma.

 

“Mradi huu unatumia njia ya Maabara za Mabadiliko (Transformation labs) ambayo inatoa fursa muhimu kwetu sote kufanya kazi kwa pamoja na kuchukua jukumu la kutafuta suluhisho la upatikanaji wa maji wenye uhakika, endelevu na usawa katika jiji la Dodoma.

                                            

 

“Tafiti na uzoefu kutoka nchi zingine kwenye maeneo yenye hali sawa na Dodoma unaonesha kuwa maji chini ya ardhi mara nyingi husaidia kupunguza madhara yatokanayo na athari za ukame na mabadiliko mengine ya tabianchi , hivyo ni matumaini yetu kuwa Mradi huu wa CLARITY utakuwa suluhisho la upatikanaji wa maji katika jiji hili”, amesema Prof. Mwatawala.

 

Akizungumzia kuhusu mradi huo Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu, na Mkuu wa Mradi huo Prof. Japhet Kashaigili amesema malengo mahususi ya Mradi wa CLARITY ni kubaini changamoto na masuluhisho bunifu kupitia utafiti wa kitaalamu katika fani tofauti ambapo malengo ya utafiti huo yanatarajiwa kufanikiwa  kupitia Maabara za Mageuzi .                                                                                                                

“Tunaposema Maabara ya mageuzi tuna maana kuwa hii ni nafasi jumuishi, salama,  ambayo wadau, watafiti na wataalamu wanakutana pamoja kufanya majaribio kupima na kubadilishana mawazo na kushirikiana katika kuzalisha maarifa na kutathmini masuluhisho”, amesema Prof. Kashaigili.


Akitoa neno katika warsha hiyo Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji kutoka Wizara ya Maji Dkt. George Lugomela amesema ili kukabiliana na hali hii kuna umuhimu mkubwa wa kufanya tafiti ili kubaini namna bora ya kusimamia vyanzo hivi vya maji ili visiendelee kuchafuliwa ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo watumishi wa wizara pamoja na bodi za maji za mabonde .

Amesema kwa kutambua umuhimu wa kufanya tafiti pamoja na kujenga uwezo mahiri kwa watumishi wa sekta ya maji, Wizara ya Maji imeanzisha Kituo Mahiri cha Rasilimali ya Maji kwa lengo maalumu la kufanya tafiti na kujenga uwezo kwa wataalamu wa Wizara , Bodi ya Maji ya Taifa na Bodi ya Maji na Mabonde katika masuala ya usimamizi na uendelezwaji wa rasilimali za maji.

Mradi wa Utafiti wa CLARITY unatekelezwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na WELL Labs (Chuo Kikuu cha IFMR Krea, India) pamoja na taasisi za utafiti nchini Uingereza (UCL, IDS Sussex, UoS, Cardiff University, British Geological Survey), Niger (Abdou Moumouni University) na Nigeria (Chuo Kikuu cha Maiduguri)

Mradi huo ambao ni wa miaka mitatu na nusu ulianza kutekelezwa mwaka 2023, unafadhiliwa na Kituo cha Utafiti wa Maendeleo ya Kimataifa (IDRC Canada), Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo (FCDO, Uingereza)  chini ya mpango wa Kukabiliana na Hali ya Hewa na Ustahimilivu (CLARE)

Picha na Tatyana Celestine, ili kutazama picha zaidi bofya link hapa chini

CLARITY FIRST T- LAB MEETING




                               

                                

Post a Comment

0 Comments