Na: Farida Mkongwe
Watanzania wametakiwa kuhakikisha
wanatunza mazingira yanayowazunguka kwa hali na mali ili kukabiliana na
mabadiliko ya tabianchi ambayo yameonekana kuleta athari kubwa katika jamii na
taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa Mei 28, 2024 na
Bi. Mwanasha Tumbo kutoka Ofisi ya
Makamu wa Rais ambaye pia ni Mratibu wa masuala ya Biashara ya Kaboni wakati
akizungumza na SUA Media kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo
kitaifa yatafanyika jijini Dodoma Juni 5, 2024.
Bi Mwanasha amesema lengo kubwa
la maadhimisho hayo ni kuhamasisha na kukumbushana faida zitokanazo na utunzaji
na uhifadhi wa mazingira sanjari na
kuelezana athari za uharibifu wa mazingira ambao umesababisha mabadiliko ya
tabianchi.
“Mabadiliko haya ya tabianchi
yametuletea mvua tusizotarajia tumeona mafuriko tusiyoyoyategemea, watu
wanakufa, mazao yanaharibika mashambani, mabadiliko haya yametuletea vimbunga
mpaka vinaitwa kina Hidaya, sasa tunatakiwa kukabiliana na athari hizo ikiwa ni
pamoja na kutunza mazingira yetu na kuzuia kuzalisha gesi joto”, amesema
Mratibu huyo.
Amesema shughuli mbalimbali
zitafanyika katika Maadhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani ikiwa ni pamoja na kampeni ya usafi
wa mazingira Kitaifa ambayo itafanyika Juni Mosi, 2024 katika maeneo mbalimbali
nchini na kuwataka wananchi kushiriki ipasavyo katika kampeni hiyo.
Maadhimisho hayo ambayo kitaifa
yatafanyika jijini Dodoma yamebeba kauli mbiu isemayo “Urejeshwaji wa Ardhi,
Ustahamilivu wa Hali ya Jangwa na Ukame ” ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
KATIKA VIDEO
0 Comments