SUAMEDIA

Wabunifu SUA wahakikishe bidhaa zao zina viwango vya juu kukidhi soko la ajira

Na: Winfrida Nicolaus

Watafiti na Wabunifu kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) waliofadhiliwa chini ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) kwa kushirikiana na Mradi wa Ubunifu (Innoversity Project) katika kuwasaidia kuendeleza Tafiti na Bunifu zao wametakiwa kuhakikisha wanakuwa na bunifu zenye viwango vya juu zinazokidhi soko la ajira na kuendana na dunia.


Amebainisha hayo Mkurugenzi wa Shahada za Uzamili, Utafiti, Uhauwilishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu SUA Prof. Japhet Kashaigili wakati akizungumza na SUAMEDIA kwenye tukio la kuziangalia bunifu mbalimbali ambazo zimefanywa na wabunifu na watafiti wakiwemo wanafunzi kutoka SUA.

Prof. Kashaigili amesema watafiti na wabunifu hao  wanatakiwa kuhakikisha wanaboresha kazi zao ili kuziharakisha kuingia sokoni na kuwa mkombozi kwa jamii inayowazunguka hasa wakulima.

Aidha ameongeza kuwa licha ya changamoto ya upatikanaji wa vifaa na  usalama wa bunifu zao bado amepeleka pongezi zake kwa Mradi wa HEET kwa kazi nzuri wanayoifanya na kusema kuwa bila kuwaunga mkono wasingefikia mahali walipo hivi sasa na kufanya wanachokifanya.

“Tumeangalia bunifu zipatazo tisa (9) ambazo kwa kuziangalia na kusikiliza ufanyaji kazi wake zinaenda kujibu moja kwa moja mahitaji ya jamii hasa wakulima ambapo tumeona mifumo ya umwagiliaji lakini pia kupima kiasi cha mbolea kwenye shamba na mbegu pia hivyo niwatie moyo kuendelea kufanya kazi kwa nguvu kuhakikisha mnaziboresha hizo tafiti na bunifu zenu”, amesema Prof. Kashaigili.

Kwa upande wake Mratibu wa Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu Kutoka SUA Dkt. Doreen Ndossi amesema kati ya bunifu ambazo wameziangalia kuna zile ambazo bado zipo hatua za awali lakini nyingine zimesonga kiasi kwamba zinaweza zikafika mahali wakasema sasa wanahitaji kuzitunza,kuzilinda na hata kuzipeleka sokoni ili kutatua changamoto katika jamii.

Aidha ametoa pongezi kwa watafiti na wabunifu hao kwa kile walichokifanya ambapo wengi wao wameenda na bidhaa zinazojibu matatizo ya jamii moja kwa moja lakini pia viwanda na kusema kuwa yawezekana kwa wakati huu vitu hivyo havijazoeleka sana sokoni lakini wakiviendeleza na kuvipeleka sokoni SUA itaweza kujivunia.








 

Post a Comment

0 Comments