SUAMEDIA

Waandishi wa habari Morogoro wapanda miti kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi

 

Na: Siwema Malibiche

Waandishi wa habari wameaswa kuendelea kushiriki katika utunzaji wa mazingira hasa upandaji wa miti katika vyanzo vya maji  ili kusaidia kukabiliana na athari za  mabadiliko ya tabianchi  kwa ajili ya vizazi vilivyopo na vijavyo.


Rai hiyo imetolewa na Katibu Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoa wa Morogoro (MOROPC) Bi. Liliani Lucas Kasenene  wakati wa  zoezi la upandaji miti ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari mkoani hapo ambapo wanahabari wamepanda miti zaidi ya 150 pembezoni mwa mto  Lukulunge uliopo kata ya Mzinga  kwa lengo la kuendelea kutunza vyanzo vya maji.


Bi. Liliani amesema mwaka huu MOROPC imeamua kuadhimisha siku hiyo kwa kupanda miti ili kuendana na Kauli Mbiu ya Maadhimisho hayo   kitaifa kwa mwaka 2024 iliyosema “Waandishi wa Habari  na Mabadiliko ya Tabianchi”.

Aidha amesema kuwa wanahabari wana nafasi kubwa ya kuielimisha jamii katika suala la utunzaji wa  mazingira huku akisisitiza  kuwa suala la upandaji miti litakuwa ni jambo endelevu kwa waandishi hao.

Kwa upande wake Pato Haule Mtumishi kutoka Bonde la Wami Ruvu mkoani Morogoro  amewapongeza waandishi wa habari walioshiriki katika zoezi la upandaji wa miti  na amesema kama Bodi itaendelea kushirikiana nao  ili wananchi waendelee kupata maji safi na ya uhakika  ili kuendeleza shughuli nyingine za kiuchumi.

Pia amewataka wakazi wote wanaoendesha shughuli zao za kiuchumi kando ya mito kuacha shughuli hizo huku akiahidi kuwa wataendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuhifadhi na kutunza vyanzo vya maji.

Naye Mwenyekiti  wa Kikundi cha  Wahamasishaji Tanzania  wanaofanya kazi chini ya Bonde la Wami Ruvu iliyoko chini ya Wizara ya Maji  Abubakari Miraji Sisango amewapongeza waandishi wa habari kwa kuamua kushiriki katika upandaji wa miti na ametoa wito kwa wakazi wote walioko karibu na vyanzo vya maji kutunza vyanzo hivyo kwa manufaa ya vizazi vijavyo huku akisisitiza kuwa kila tone la maji nchini linapaswa kuhifadhiwa.

Baadhi ya Waandishi wa habari walioshiriki zoezi hilo la upandaji miti akiwemo Bibi. Elizabeth Tanzania wamesema ni  jambo zuri kwa waandishi kushiriki katika upandaji wa miti ili kusaidia harakati za kupambana na  mabadiliko ya tabia nchi  kwa sababu mazingira yanapoharibika waathirika wake ni jamii yote kwa ujumla wakiwemo wanahabari.

Kassim Abdul Chunga  mkazi wa  kata ya Mzinga amewashukuru wanahabari wote waliojitokeza katika upandaji wa miti karibu na mto huo na  amekiri kuwa  wamekuwa wanapatiwa  elimu ya kutunza mazingira mara kwa mara na hivyo kuwataka wanajamii wenzake kuzingatia maelekezo wanayopewa na wataalam wa mazingira.






Post a Comment

0 Comments