SUAMEDIA

Ufadhili wa Samia kusomesha wanafunzi bora wa Sayansi kwa asilimia 100

 Na: Gerald Lwomile

Serikali imesema wanafunzi watakaomaliza kidato cha sita na kufaulu vizuri masomo ya Sayansi, watasomesha bure kwa asilimia 100 na Serikali kupitia ufadhili wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda akisisitiza jambo wakati wa ufunguzi wa Madhimisho ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu.

Hayo yamesemwa leo Mei 26, 2024 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda, wakati wa ufunguzi wa Madhimisho ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu inayofanyika jijini Tanga.

Prof. Mkenda amesema katika kuhakikisha wanatekeleza mpango huo wameanzisha Ufadhili wa Samia yaani ‘Samia Scholaship’ ambao utasomesha bure pasipo mkopo wanafunzi bora wa mwanzo kati ya 600 hadi 700 na watachagua kama wanataka kusoma vyuo vya ndani au vya nje.

Amesema maeneo yaliyopewa kipaumbele ni nyanja za Sayansi, Uhandisi, Elimu Tiba na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ambapo wanafunzi hao watasomeshwa bure kwa asilimia 100, kupewa fedha za kujikimu, vitabu na huduma zote muhimu.

Akizungumzia kuhusu kuchochea ubunifu, Prof. Mkenda amesema kumekuwa na malalamiko kuwa Serikali haiwajali wabunifu jambo hilo si kweli kwani Wizara yake imekuwa ikiwataka watu kuendelea kufanya ubunifu na kuupeleka ubunifu huo kwao na ule utakaoonekana una manufaa utapatiwa fedha ili uendelezwe.

Makamu Wakuu wa Vyuo na Wakuu wa vyuo mbalimbali wakisikiliza hotuba ya Mgeni rasmi 

Akizungumza kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi amesema ili kuhakikisha Tanzania inapiga hatua ni muhimu kuwa na watu wenye ujuzi na wabunifu.

Amesema wabunifu kutoka nje ya nchi pekee ni hatari kwa taifa kwani  hawawezi kuwa na uchungu na nchi hii kwani wanajua wao ni wapitaji hivyo lazima kama taifa lipate wataalamu wabobezi katika ujuzi na ubunifu.

Amesema Serikali imetenga  zaidi ya shilingi bilioni 3 ili kufufua vyuo,  na zaidi ya shilingi bilioni 3.4 kujenga vyuo vipya, huku akisisitiza kuwa hiyo ndiyo njia ya kutatua changamoto zinazolikabili taifa.                                                                                

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo Madhimisho ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu.

Akitoa taarifa ya Maadhimisho ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema Maadhimisho ya mwaka 2024, yameshirikisha zaidi ya Taasisi 140, wabunifu ambao ni washindi wa Makisatu 20. vyuo vya ufundi 27, ufundi stadi na wanafunzi shule za sekondari.



Picha chini ni viongozi mbalimbali  waliofika katika Banda la SUA 






                              




Post a Comment

0 Comments