SUAMEDIA

Waajiri kote nchini waaswa kuzingatia maagizo ya Serikali

 

Na:Tatyana Celestine-Mwanza

Serikali imewataka waajiri kote nchini kutekeleza maagizo yanayotolewa kuhakikisha Waandishi Waendesha Ofisi wanafanyakazi kwa kuzingatia Taaluma, Muundo, majukumu yanayowahusu katika utendaji kazi pamoja haki ya kuudhuria mikutano ya TAPSEA.

                                

Hayo yamesemwa kabla ya kumruhusu mgeni rasmi kuzungumza katika Ufunguzi wa Mkutano wa 11 wa Kitaaluma Tanzania (TAPSEA) jijini Mwanza na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Mhe. George Simbachawene kuwa kuna waajiri ambao hawatekelezi maagizo yanayotolewa na Serikali hivyo wakiendelea kukaidi watachukuliwa hatua.

Waziri Simbachawene akijibu Risala iliyosomwa na Mwenyekiti wa TAPSEA Bi. Zuhura Songambele ikizungumzia changamoto wanazokutana nazo katika mahala pa kazi ambapo imesikilizwa pia na viongozi mbalimbali wa Serikali waliojumuika kumsindikiza Mgeni Rasmi akimuwakilisha Rais wa Jamhuriya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Naibu Waziri Mkuu Dkt. Doto Biteko katika ufunguzi huo jijini Mwanza leo.

                               

Waziri huyo amesema kutokana na mabadiliko yaliyofanywa na serikali kupitia chama chao kada hiyo kwasasa inatoa taaluma mpaka ngazi ya shahada hivyo amewataka waajiri kuzingatia muundo na majukumu yanayowahusu katika utendaji kazi na sio kuwaweka katika shughuli ambazo tofauti na taaluma yao sambamba na hilo ameahidi kutoa walaka wa kuonyesha majukumu yao na watambulike kama wasaidizi wa ofisi za viongozi na sio waandishi pekee.

Aidha Mhe. Simbachawene amebainisha kuwa katika kushughulikia changamoto hizo Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeanzisha Mobile Clinic katika mkutano huo ambapo waandishi waendesha ofisi  wamepata fursa ya kukutana na wataalam kutoka Ofisi hiyo imepelekea kwa kiasi kikubwa kuweza kutatua changamoto hizo kama vile kuuisha muundo wa kada yao ambao umeanza kutumika July 2023, kutoa nafasi za ajira 722 kwa kada hiyo, waandishi waendesha ofisi 864 wamepandishwa vyeo na kuidhinishiwa mishahara na kulipa malimbikizo  ya madai yao.

                           

Akimwakilisha Rais Samia, Naibu Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa wizara husika imeanza kushughulikia changamoto hizo kama alivyoelezea Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Mhe. George Simbachawene lakini kwa upande wake amesema amepokea mapendekezo sita ambayo yamewasilishwa na kwamba watashughulikia mapendekezo hayo kikamilifu ikiwemo baadhi ya waajiri kutowapangia majukumu kulingana na taaluma yao, kutowalipia kwa wakati malipo ya kushiriki mikutano ya TAPSEA, Waajiri kutotekeleza muundo mpya katika kada hiyo na kutotumia muundo huo katika kuwapangia kazi zinazoendana na taaluma yao.

                        

Aidha Mhe. Dkt. Biteko amewaomba waandishi waendesha ofisi kuzingatia uadilifu na uaminifu katika kazi kwani ndiyo njia rahisi ya kuonesha umuhimu na mabadiliko kwa muajiri wao na kuachana na tabia zisizofaa ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na watu wengi huku akiwataka kutambua kwa sasa wanatakiwa waendane na sayansi na teknolojia kulingana na mabadiliko yaliyopo hivyo wajielimishe namna ya kutumia teknolojia mpya zinazotumika katika kazi zao kama vile vishikwambi na komputa.

Awali akiwakaribisha wageni kutoka maeneo mbalimbali ya nchi kufika katika Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda amevishukuru vyombo vya usalama kuhakikisha hakuna changamoto yoyote iliyotokea kwa wageni lakini amewataka kutembelea vivutio ambavyo vipo jijini Mwanza kwani Mkoa huo unachangia pato la taifa kupitia vivutio hivyo.

Aidha ameishukuru Serikali ya Rais Samia kwa kufanya mambo makubwa katika mkoa huo akiyataja machache yakiwemo kupitia Wizara ya Nishati kwenye Mradi wa REA awamu ya pili ambapo Serikali imetoa sh. bilioni 56,  kupitia Program ya ujazilizi wa umeme Serikali imetoa bilioni 12 na  Mradi wa Pre Urban Serikali imetoa  sh. bilioni 8, pamoja na hilo pia imefanya upanuzi wa uwanja wa Ndege, Ujenzi wa Daraja, Ujenzi wa meli ya kisasa, kuleta vivuko vitano  na kuwepo kwa maji ya kutosha kupitia Mradi wa Maji wa Butimba.                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                  















Post a Comment

0 Comments