Na: Ayoub Mwigune
Zaidi ya wanafunzi 600 kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wameshiriki katika Kongamano lililoandaliwa na Ushirika wa Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUGECO) la kuwawezesha kutambua fursa mbalimbali zilizopo katika kilimo biashara sambamba na kupata mafunzo kwa vitendo nje ya nchi.
Akizungumza na SUAMEDIA Bw.
Revocatus Kimario ambaye ni Mkurugenzi wa SUGECO amesema dhima ya kongamano lililoandaliwa na
SUGECO ni kuwakutanisha wanafunzi waliomaliza na ambao wanaendelea na masomo
kwa ajili ya kuwaelezea fursa mbalimbali zilipo katika kilimo biashara ambazo
zinatolewa na Ushirika huo pamoja na wadau wake.
Kimario amesema tangu kuanzishwa kwa SUGECO, imekuwa ikipeleka vijana mbalimbali
wahitimu wa SUA nje ya nchi hasa katika mataifa ya Ulaya, Amerika na Asia ambapo
hujifunza namna nzuri ya kufanya kilimo chenye tija lakini mchakato huo
huhitaji fedha za awali kumwezesha mhitimu husika kujiandaa ipasavyo.
Amesema katika kuhakikisha wanaondoa changamoto
mbalimbali ambazo zimekuwa zikiwakwamisha vijana kukosa fursa ya kwenda nje ya
nchi ili kujifunza kwa vitendo na
kutambua fursa za kilimo biashara SUGECO wamesaini mkataba na Benki ya CRDB
kupitia ‘CRDB Foundation’ ambao utawawezesha zaidi ya wahitimu 2,500 SUA na
vyuo vingine kunufaika na fursa hizo.
Kwa upande wake Bw. Joseph Masimba
ambaye ni Mkurugenzi wa Ubunifu na Uendeshaji SUGECO
ameishukuru SUA kwa namna ambavyo imekuwa ikishirikiana na ushirika huo ambapo
kupitia ushirikiano huo umewezesha SUGECO kuendelea kuwajengea uwezo vijana
wengi chuoni sambamba na kuwapa fursa mbalimbali katika kuhakikisha vijana
wanajifunza katika mataifa mbalimbali ili kuweza kubaini fursa na kuongeza
mtandao katika kilimo.
Naye Rachel Mkwizu mwanafunzi wa mwaka wa pili SUA kutoka Ndaki ya
Kilimo anayechukua Shahada ya Sayansi ya Udongo na Mimea amesema kupitia
kongamano hilo amekuza uelewa kuhusu namna ya kutambua
soko katika kilimo pamoja kuona ni namna gani anaweza kukuza ujuzi wake kwa
vitendo katika mataifa mbalimbali sambamba
na kujiajiri kupitia kilimo.
Kwa upande wake
muwakilishi wa Benki ya CRDB ambao ni wadau wa SUGECO Bi. Shallon Nsule amesema taasisi ya CRDB
Foundation imekuwa ikitekeleza Program ya Imbeju inayotoa mafunzo ya
ujasiriamali pamoja na mtaji wezeshi kwa vijana na wanawake na hivyo imefurahi
kuingia ushirikiano na SUGECO ambapo kupitia ushirikiano huo vijana wengi watanufaika
na program hiyo.
0 Comments