Na: Tatyana Celestine
Kutokana na ukuaji wa Sayansi na Teknolojia katika
Kilimo duniani Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kinaendelea kuwafundisha
wanafunzi wake kwa vitendo kupitia mashamba na bustani za Kilimo cha Matunda na
Mboga namna bora ya kuweza kutumia fursa hiyo ili kuwa bora katika ajira
au kujiajiri wenyewe.
Akizungumza na SUA MEDIA kuona namna ambavyo matumizi ya Teknolojia za Kilimo zinawezaje kumsadia mwanafunzi awapo katika mafunzo kwa vitendo chuoni hapo, Afisa Kilimo Mwandamizi toka Idara ya Mimea Vipando na Bustani Bw. Godwin Rwezaula amesema kuwa Chuo kinaendelea kuboresha na kuongeza vitendea kazi kulingana na mahitaji ya ufundishaji kutokana na hali ya sasa wanafunzi wanatakiwa kuzifahamu teknolojia mpya na matumizi yake hata kabla hawajahitimu.
Afisa Kilimo huyo ameongeza kuwa suala la
kuamua wanafunzi kufanya Mafunzo kwa Vitendo chuoni hapo limekuwa na faida kwa
wanafunzi hivyo kupelekea idadi ya wanafunzi kuongezeka ambapo zaidi ya
wanafunzi elfu mbili kutumia mashamba na bustani za chuo kwa kufanyia Tafiti na
Kilimo tofauti na miaka ya nyuma.
Naye Mwanafunzi wa Mwaka wa Tatu wa Shahada ya Kilimo
kwa Ujumla chuoni hapo Bw. Hassan Mohamed ameelezea faida wanayopata kupitia
chuo hicho na kusema kuwa mafunzo hayo yanayozingatia ulimwengu wa Teknolojia
katika upande wa kilimo kwao ni faida ambayo inawafanya wakimaliza masomo yao
kuweza kuelimisha jamii kuhusiana na umuhimu wa kutumia teknolojia katika
kilimo kutokana na maeneo wanayotoka elimu hiyo haipo zaidi wanalima kimazoea.
Amezitaja faida wanazozipata kama vile mafunzo
ya kutumia mbegu sahihi, Kilimo na Uvunaji
wenye tija, kurahisisha umwagiliaji maji au dawa kwa kutumia ndege (drone),
kuongeza uzalishaji wa mazao, utambuzi wa vifaa vya kurahishia kazi, pamoja na
kutunza mazingira kwa kuacha kuchoma moto eneo kwa matumizi ya kilimo.
Aidha Bw. Mohamed amesema kuwa elimu wanayopata
itasadia kuwakumbusha wazazi watumie fursa hiyo ya ukuaji wa teknolojia kwa
kuwafanya watoto wao wajiunge na SUA kusomea kilimo kwani Sekta ya Kilimo kwa sasa
inahitaji watu walioelimika hata kama hawakuweza kuajiriwa wawe wanauwezo
kujiajiri wenyewe na kuepukana na utegemezi kwa kusubiri ajira.
Aidha amewaasa wanafunzi wenzake kutambua kuwa
wao ni mabalozi kutoka SUA hivyo kufanya kwao kazi vizuri katika jamii ndio
inaleta hamasa kwa wengine kupenda kilimo wasione shida kujitolea kufanya kazi
hizo kwani zinawajenga kuwa bora.
0 Comments