SUAMEDIA

SUA yaahidi kuboresha maslahi ya wafanyakazi wake

 

Na: Siwema Malibiche, Tatyana Celestine

Menejiment ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) imeahidi kuboresha maslahi ya wafanyakazi kulingana na bajeti kwa kuanza na wafanyakazi waendesha ofisi, wahudumu na Usalama katika chuo hicho kwa kuwaongezea kipato (Posho) kwa lengo la kuwafanya waongeze bidii, nidhamu na uaminifu katika kazi zao.

                               

Akizungumza na wafanyakazi katika kilele cha Siku ya Wafanyakazi Mei Mosi Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda amesema kada hizo zimekuwa zikifanya kazi lakini mapato yao ni madogo hivyo kwa kuhakikisha nao wanaweza kupata ongezeko, Chuo kimeamua kuanza nao wakati kikiendelea kujipanga hadi kufikia kila mfanyakazi katika kada nyingine chuoni hapo.

Akijibu ombi la wafanyakazi kupatiwa usafiri lilisomwa katika Risala yao Prof. Chibunda amesema kuwa tayari chuo kimeendelea kuongeza mabasi kwa ajili ya wanafunzi na kufikia saba lakini pia wameona kuna uhitaji wa kuongeza zaidi kwa wafanyakazi kulingana na gharama za maisha na nauli kupanda ili kila mfanyakazi apate huduma ya usafiri.

Aidha amesema kuwa yote hayo Menejiment inafanya lakini wanataka kuona wafanyakazi wanafanya kazi kwa bidii, Uaminifu,Uadilifu na Uzalendo katika chuo hicho, na kusema kuwa wafanyakazi watambue wanawajibu kufanya hivyo na sio suala la kusukumwa katika kuwahi kufika kazini, kuhakikisha wanafanya kazi kikamilifu, pamoja na kufahamu utaratibu wa kupata likizo na malipo ya likizo zao ili kuepuka malalamiko mbalimbali.

Prof Chibunda pia amewapongeza wafanyakazi Bora 74 wakiwemo Wanataaluma na Waendeshaji katika chuo hicho kwa kuwapatia zawadi ya fedha na vyeti ambapo  wengine wawili kati yao ambao ni wafanyakazi Bora wa Chuo wamepata zawadi katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi ki mkoa yaliyofanyika wilayani Ifakara mkoani Morogoro na  kusisitiza  kila mfanyakazi katika nafasi yake kuwajibika ipasavyo ili kuleta maendeleo ya chuo na Taifa kwa ujumla.                                   

Kwa upande wao Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi chuoni hapo Mwenyekiti wa Chama cha wafanyakazi RAAWU Bw. Faraja Kamendu na Mwenyekiti wa THTU Dkt. Nickson Mkiramweni wamewataka wafanyakazi kujiunga na vyama vya wafanyakazi kwani kuna manuufaa katika kupambania haki na usawa wa wafanyakazi na kusema kuwa wafanyakazi waliopata zawadi ikawe motisha kwa wafanyakazi wengine kuendelea kujituma kazini. 









Picha na Nicholus Roman

 Katika Video

Post a Comment

0 Comments