Na: George Joseph
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan leo amefanya uzinduzi wa kimkakati wa
taifa wa nishati safi ya kupikia ya mwaka 2024 mpaka 2034 katika Kituo
cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini
Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan akitete jambo na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mheshimiwa Dkt Dotto Biteko (Picha Ikulu) |
Mhe Rais amesema tatizo la
matumizi ya nishati safi ya kupikia ni la mtambuka na lengo la pamoja, hivyo
mkakati huu utasaidia kupunguza gharama za nishati safi na pia uharibifu wa
mazingira ambapo hekta laki 4 na 66 elfu za misitu zinateketea kila mwaka.
Amebainisha kuwa watanzania
wapatao elfu 33 hupoteza maisha kila mwaka kwa magonjwa yasababishwayo na
maradhi ya kupumua ambapo chanzo chake ni uvutaji wa moshi wa nishati isiyo safi
ya kupikia.
Vilevile Mhe. Rais ameiomba sekta
binafsi kuleta teknolojia mpya ya nishati ya kupikia ikiwezekana ile ya
matumizi ya kulipia kadri utumiavyo kama ilivyo katika nishati ya umeme, na
serikali itatoa ushirikiano katika hilo ili kupunguza gharama na kumuwezesha
kila mtanzania aweze kumudu gharama za matumizi.
Rais Samia amemuagiza Waziri Mkuu
Mhe. Kassim Majaliwa pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na
Mazingira Mhe. Suleiman Jaffo kwa miezi mitatu ijayo waandae katazo rasmi la
kuzuia taasisi zote nchini zenye kuhudumia watu zaidi ya 100 kutokutumia
nishati ya kuni na mkaa katika matumizi
Akizungumza wakati wa hafla hiyo Mhe.
Suleman Jaffo amesema zaidi ya watu milioni 2 barani Afrika wanafariki kwa
sababu ya matumizi ya nishati isiyo safi kwa kupikia.
Jaffo amesema idadi kubwa ya
taasisi mbalimbali kubwa hapa nchini kwa sasa zimeanza kutumia nishati inayofaa
zikiwemo Magereza, vyuo vikuu mbalimbali ambayo ni idadi ya vyuo vikuu 30 kati
ya 35 kwa sasa vinatumia nishati safi ya
kupikia katika shughuli zake.
Akitoa salaam kwa niaba ya Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Spika wa Bunge hilo Mhe. Dkt Tulia Akson, amesema Bunge linamuunga
mkono Mhes. Rais katika maendeleo ya kimkakati ya nishati safi ya kupikia iliyo
na lengo la kumkomboa mwanamke kiuchumi kwa njia ya kupunguza muda mwingi
anaoutumia kutafuta nishati safi ya kupikia.
Nae Naibu Waziri Mkuu na Waziri
wa Nishati Mheshimiwa Dkt Dotto Biteko amesema serikali itaendelea kuzuia
matumizi ya nishati isiyo safi na lengo ni mpaka kufikia mwaka 2030 asilimia 80
ya watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.
Uzinduzi huo umefanyika na
kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, viongozi wa dini, sekta binafsi,
wafanyabishara na jumuiya mbalimbali za wanawake nchini.
0 Comments