Na: Tatyana Celestine
Chuo Kikuu cha Sokoine cha
Kilimo (SUA) kimeendelea kudhihirisha ubora wake katika Tafiti, Kilimo na
ufundishaji kiasi cha kuvutia watu kutoka Kisiwa cha Mayotte kilicho chini ya
nchi ya Ufaransa karibu na nchi za Madagascar na Comoro kufika ili kuomba ushirikiano
wa ufundishaji, Tafiti, Ushauri wa kitaalamu, Teknolojia mpya na uzalishaji ili
kuinua hali ya kilimo kwa nchi yao.
Akizungumza na SUA Media Rais
wa Chama cha Kusaidia katika Kilimo ‘Association Moussada Fampitahitahy
N'tobi’ (AMFT) Bi. Zakianti Dhurari amesema kuwa SUA ni Chuo
kilichopo Tanzania nchi yenye amani na usalama hivyo wameshawishika kufika kwa kuamini
SUA itawasaidia kutatua changamoto ya kilimo nchini kwao kutokana na
ufinyu wa eneo huku idadi ya watu ikiongezeka.
Aidha amesema kuwa ujio
wao umewapa matumaini makubwa kwani SUA imeonyesha nia ya kukubali kuwa washirika
wa nchi yao katika nyanja za kilimo, utafiti, pamoja na kubadilishana ujuzi
katika teknolojia bora ambazo zitasaidia kwa kubadilishana
wanafunzi wa pande hizo mbili.
Naye Katibu Mkuu wa Chama
hicho Bw. Boinali Said amesema, baada ya kufika SUA amegundua kuna fursa
nyingine nyingi ambazo wangependa kuzitumia kama vile kusafirisha mazao ya
kilimo kwenda nchini kwao lakini pia kuhamasisha watu wa nchi yao kuja
kujifunza zaidi kuhusu kilimo kupitia SUA kutokana na kuwa na wabobezi na
wataalamu wengi chuoni hapo.
Amesema pamoja na mambo mengine
wanategemea kujenga majengo ambayo yatasaidia wanafunzi kutoka kwao lakini pia
majengo hayo yatatumia na wanafunzi wengine nchini na wataishi kwa amani kama watoto
wa familia moja na hivyo hivyo wanafunzi wa SUA wakienda nchini mwao watapata
fursa ya kujifunza lugha ya Kifaransa kwani wako tayari kutoa elimu hiyo kwa
wanafunzi wa SUA.
Kwa upande wake Mkurugenzi
wa Kurugenzi ya Shahada ya Uzamiri , Utafiti, Uahulishaji wa Teknolojia na Ushauri
wa Kitaalam Prof. Japhet Kashaigili amesema kuwa ugeni huo kutoka kisiwa cha
Mayotte wamekichagua chuo hicho kwa kuona wanaweza kupata taarifa nyingi ambazo
zitawafikisha katika malengo yao na hali hiyo inakiweka chuo chao katika nafasi
ya kusaidia ndani na nje ya nchi.
“Taasisi hiyo inahitaji la kuinua hali ya
kilimo katika nchi yao hivyo taasisi hiyo imelenga zaidi katika tafiti na
kubadilishana wanafunzi, tafiti katika madawa ya asili, uzalishaji wa miti na kilimo kwa ujumla hizo ni hatua za awali,
hatua zifuatazo ni kuanza mchakato wa makubaliano na baadae ni kufanya
utekelezaji.” amesema Prof. Kashaigili.
0 Comments