SUAMEDIA

Dawa ya Miti Shamba kutafitiwa ili itibu ugonjwa wa Homa ya Kiwele kwa wanyama

 Na: George Alexandar

Imeelezwa kuwa ugonjwa wa Homa ya Kiwele ni hatari kwa mnyama na hupelekea kuleta hasara kwa mfugaji kwa kuwa matibabu yake ni gharama, yanachukua muda mrefu na hunasababisha upotevu wa maziwa.


Prof. Gaymary Bakari  ambaye ni Naibu Rasi wa Ndaki ya Tiba ya Wanyama na Sayansi za Afya SUA

Hayo yamesemwa na hivi karibuni katika uzinduzi uliofanywa jijini Dar es Salaam na Prof. Gaymary Bakari  ambaye ni Naibu Rasi wa Ndaki ya Tiba ya Wanyama na Sayansi za Afya  na Mkuu wa Mradi huo wakati wa uzinduzi wa Mradi wa tafiti za kibunifu kwa kutumia utomvu wa miti shamba kutibu ugonjwa wa Homa ya Kiwele kwa Wanyama wanaozalisha Maziwa, ambapo ameongeza kuwa mradi huo utahusisha watafiti kutoka takribani nchi tatu ambazo ni Kongo, Kanada na Tanzania.

Amesema watafiti kutoka mataifa mengine pia watatumika katika kupima sampuli mbalimbali kulingana na upatikanaji wa vifaa katika nchi zao ambapo watafiti hao watasadia pia kuwafundisha watafiti wengine, wataalamu wa maabara pamoja na wanafunzi wa SUA.

Katika maelezo yake Prof. Gaymary amesema uzinduzi wa mradi huo unakuja na uzinduzi wa dawa za mitishamba ambazo zitakuja kuwapunguzia gharama za kimatibabu wafugaji, ambapo kwa sasa kumekuwa na gharama kubwa katika kukamilisha matibabu hivyo kupelekea wafugaji kushindwa kumaliza matibabu ya ugonjwa huo na kusababisha mnyama kupunguza wingi wa maziwa anapokamuliwa.

Prof. Gaymary ameongeza kuwa kupitia mradi huo wakulima watanufaika kwa kupata elimu kutoka kwa watafiti wa ndani na nje ya nchi, huku akiwataka wafugaji nchini kuwa tayari na mapokeo ya matokeo ya watafiti juu ya namna ya kupambana na magonjwa kwa wanyama ikiwemo ugonjwa huo wa Kiwele.



Post a Comment

0 Comments