Na, Winfrida Nicolaus
Balozi wa Ubelgiji nchini Tanzania Mhe. Peter HuygheBaert amesifu na kuridhishwa na kazi inayofanywa na
Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) pamoja na Kituo cha Utafiti
cha Mradi wa Apopo katika
kuhakikisha wanatatua changamoto mbalimbali kwenye jamii ya Kitanzania ikiwemo
kuwatumia panya katika utatuzi wa magonjwa kama vile Kifua Kikuu (TB)
Akizungumza na SUA Media Balozi huyo amesema kufanya
kazi na SUA inamaanisha wanafanya kazi na nchi nzima ya Tanzania hivyo
ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo mbili ni wa manufaa makubwa na wakiwa kama
wafadhili wakubwa wa Mradi wa APOPO inaleta hamasa na kufurahisha kuona
ushirikiano huo unafanya kazi nzuri katika utatuzi wa changamoto mbalimbali.
“Kile tulichokiona kinavutia sana kutokana na ushirikiano uliopo kwanza
kabisa baina ya SUA na Chuo chetu cha Antwerp na baadaye kushirikiana katika Mradi ambao
unavutia sana wa kutumia Panya katika matumizi mbalimbali lengo likiwa kuifanya
jamii kuwa salama”, amesema Balozi huyo
Kwa upande wake Mhadhiri kutoka SUA Prof.
Abdul Katakweba akimwakilisha Prof. Allen Malisa Mkurugenzi wa Taasisi ya Kudhibiti Viumbe Hai
Waharibifu amesema APOPO inafanya kazi chini ya Taasisi ya SUA lakini pia kuna
ushirikiano baina ya SUA, APOPO pamoja na Chuo Kikuu cha
Antwerp kilichopo nchini Ubelgiji.
Amesema APOPO ni Taasisi isiyo ya Kiserikali kutoka
nchini Ubelgiji na huo ubalozi ndio unaofadhili sehemu kubwa katika tafiti
zinazofanywa na Taasisi hiyo pamoja na SUA hivyo ujio wa balozi huyo ni
kujiridhisha kwa kuangalia endapo misaada inayotolewa na nchi yao kama inafanya
kazi vizuri au lah! na kitu kizuri ni kuwa kazi imeonekana.
“Ushirikiano
wetu mkubwa kati ya APOPO na SUA ni ufanyaji wa Tafiti katika kusaidia binadamu
kwa ndani ya nchi na nje ya Tanzania ambapo tunatumia panya kunusa mabomu
lakini pia makohozi kwa ajili ya kubaini vimelea vya Kifua kikuu na kwa upande
wa Tanzania tafiti hiyo imekwenda vizuri sana ambapo tuna hospitali zaidi ya 58
ambazo panya hao wanaweza kutumia makohozi
ili kuweza kubaini vimelea hivyo”, amesema Prof. Katakweba
Katika Ziara hiyo Balozi huyo ametembelea maeneo
mbalimbali ikiwemo Maabara ya kutambua vimelea vya Kifua Kikuu (Morogoro TB
Detection), Shamba la Mfano la Mafunzo la Kilimo Msitu, Eneo la Mafunzo ya
Panya wanaokabiliana na majanga ikiwemo kutegua mabomu na baadaye Ofisi ya
Makamu wa Mkuu wa Chuo cha SUA.
0 Comments