Na: Gerald Lwomile
Serikali imesema kazi nyingi za
wabunifu nchini zina matokeo chanya jambo ambalo litalisadia taifa kuhakikisha
linasonga mbele na kutatua changamoto mbalimbali.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza katika kilele cha Madhimisho ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu (Picha zote na Gerald Lwomile) |
Hayo yamesemwa Mei 31, 2024 na
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa wakati
akiahirisha Maadhimisho ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu iliyofanyika jijini
Tanga.
Mhe. Majaliwa amesema ameshuhudia
ubunifu wa hali juu katika wiki hiyo ikiwemo vijana watafiti mbalimbali ambao
wamekuja na teknolojia na ubunifu mbalimbali ambao utasaidia taifa kutoagiza
vifaa nje na kutumia fedha nyingi za kigeni.
“Nimeona kijana mmoja kutoka VETA
ametengeneza chombo kinachokuza sauti na kumuwezesha mwenzetu ambaye hasikii
vizuri, mwenye usikivu hafifu kusikia vizuri, sasa kama unaweza kutengeneza
ukabuni chombo kama hiki na huku tukitambua kuna watanzania wana matatizo ya
kusikia tayari umeshapata soko” amesema Mhe, Majaliwa.
Akielezea mipango ya Serikali
katika kukuza utafiti, ujuzi na ubunifu Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa amesema Serikali
itaendelea kuweka nguvu katika eneo hilo ili lilete tija nchini.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha
Waziri Mkuu, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda ameishukuru
Serikali kwa kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wote wanaosoma masomo ya
Sayansi.
Prof. Mkenda amesema ufadhili huo
utachochea na kutoa hamasa kwa vijana wengi kusoma masomo ya Sayansi, Uhandisi,
Elimu Tiba, Hisabati na TEHAMA.
Wakati huo huo Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia imetoa zawadi na vyeti kwa watafiti mbalimbali ambao
wametoa machapashio yao na kufanya vizuri kwenye majarida makubwa ya kisayansi duniani.
Miongoni mwao ni Marehemu Prof.
Ludovick Kazwala kutoka SUA ambaye zawadi yake na cheti kilipokewa na familia
yake ikiongozwa na mkewe Bi. Lydia Kazwala, mwingine ni Prof. Hezron Nonga kutoka
Ndaki ya Tiba ya Wanyama na Sayansi Shirikishi.
Mke wa Marehemu Prof. Kazwala Bi. Lidya Kazwala akipokea cheti kutoka kwa Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa. |
Maadhimisho ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yalianza Mei 25, 2024 na kufikia kilele Mei 31, 2024, maadhimisho hayo yalibebwa na kauli mbiu isemayo ‘Elimu, Ujuzi na Ubunifu kwa Uchumi Shindani’
Prof. Nonga akipokea cheti kutoka kwa Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa. |
0 Comments